Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim (pichani), atafanya ziara ya kikazi nchini kuanzia tarehe 19 hadi 21 Machi 2017.

Akiwa nchini, Dkt. Kim atafanya mazungumzo na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ikulu Jijini Dar es Salaam siku ya Jumatatu, tarehe 20 Machi 2017 pamoja na kushiriki uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara za Juu katika eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).

Katika mazungumzo yao, Viongozi hao watajadili namna bora ya kuimarisha zaidi uhusiano uliopo kati ya Tanzania na benki hiyo. Vilevile, watazungumzia miradi mikubwa inayotarajiwa kutekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika kipindi kijacho.

Aidha, baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli na mgeni wake watashuhudia uwekwaji saini wa mikataba mitatu: (i) Uboreshaji Miundombinu ya Usafiri Jijini Dar es Salaam ikiwemo awamu ya tatu na ya nne ya mradi wa DART pamoja na ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la Ubungo (Dar es Salaam Urban Transport Project (DUTP); (ii) Awamu ya pili ya mradi wa Uboreshaji wa Upatikanaji wa Maji safi na uboreshaji wa miundombinu ya maji taka (Water and Sanitation Project) na (iii) Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za msingi katika baadhi ya miji (Tanzania Strategic Cities Project).

Wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kim atapata pia fursa ya kutembelea Shule ya Msingi Zanaki ambayo ni moja ya Shule zinazonufaika na mpango wa kuboresha ubora wa elimu ya msingi unaogharamiwa na Benki ya Dunia.

Ziara ya Dkt. Kim inafuatia ziara iliyofanywa nchini na Makamu wa Rais wa Benki hiyo wa Kanda ya Afrika, Bw. Makhtar Diop mwezi Januari 2017 ambapo alishiriki uzinduzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi (BRT) uliofanyika kwenye kituo kikuu cha mabasi hayo kilichopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 17 Machi, 2017
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: