KAMANDA wa polisi mkoani Pwani, Boniventure Mushongi, akizungumzia tukio la mauaji lililotokea wilayani Kibiti mkoani Pwani.
Na Mwamvua Mwinyi, Kibiti
Watu watatu wamepoteza maisha mmoja kati yao akiwa OC CID Kibiti baada ya kuuwawa na kundi la watu wanaodhaniwa ni majambazi wakiwa na silaha aina ya SMG/SAR huko eneo la Jaribu Mpakani kata ya Majawa ,Kibiti .
Tukio hilo limetokea feb 21 majira ya saa mbili usiku ambapo watu sita walivamia katika kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu na kuuwa watu watatu .
Kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ,aliwataja waliouawa kuwa ni OC CID wilaya ya Kibiti sp.Peter Kubezya ambae amepigwa risasi kwenye kiuno .
Wengine ni Peter Kitundu Mkaguzi wa maliasili kituo cha Jaribu Mpakani na mgambo aliyekuwa akifanyakazi za ulinzi kwenye kizuizi hicho, Athumani Ngambo .
Kamanda Mushongi alisema wote hao wawili waliuawa kwa kupigwa risasi kichwani na begani na kupoteza maisha papo hapo .
Aidha wakati majambazi hayo yakifanya uhalifu huo waliweza kuwaita wananchi wafike kwenye kizuizi hicho ili wachukue mkaa na mazao ya misitu .
Kufuatia wito huo wananchi walijitokeza na kwenda kujibebea mkaa na mazao hayo kisha kuondoka nayo.
“Baada ya kutokea kwa tukio hilo kundi la makachero likiongozwa na OC CID Kubezya lilifika eneo la tukio kupambana na wahalifu lakini wakiwa kwenye majibizano ya kurushiana risasi mkuu huyo wa upelelezi alijeruhiwa kiunoni ambapo alifariki akiwa njiani akielekea hospitali ya mission ya Mchukwi ” alieleza Mushongi .
Kamanda Mushongi alifafanua kwamba katika eneo la tukio kulikutwa pikipiki mbili namba MC 853 AHH aina ya Toyo na MC 799 aina ya Sunlg pamoja na kipeperushi chenye ujumbe wa kitisho .
Kutoka vyanzo mbalimbali huko Kibiti vinasema vipeperushi hivyo vinaeleza kupinga kuwepo kwa vizuizu vya mazao ya misitu wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: