WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itapambana na janga la dawa za kulevya na kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.

Ametoa kauli hiyo (Ijumaa, Februari 10, 2017) bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la 11.

“Lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na dawa za kulevya na kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na wasambazaji. Dhamira ya Serikali ni kupambana na janga hili kwa dhahiri na kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki,” amesema.

Akizungumzia idadi ya watu ambao hadi sasa wamekwishakamatwa katika nchi mbalimbali, Waziri Mkuu amesema takwimu za jumla zinaonyesha kuwa Watanzania 515 wamekamatwa na kufungwa gerezani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.

“Nchini China Watanzania walioko magerezani ni zaidi ya 200; Brazili kuna Watanzania 12; Iran wako Watanzania 63; Ethiopia Watanzania saba na Afrika Kusini wako Watanzania 296,” amesema.

Waziri Mkuu amesema moja ya hoja za Kamati za Kudumu za Bunge iliyojadiliwa na kuibua hisia kali katika mkutano huu wa Bunge ni kuhusu vita inayoendelea nchini dhidi ya dawa za kulevya na akawaomba Watanzania wote waiunge mkono Serikali juu ya vita hiyo.

“Watanzania wote ni mashahidi kwamba vijana wetu wengi wameendelea kudhoofika kiafya kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii inayopiganwa sasa dhidi ya uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo,” amesisitiza.

Amesema dawa hizo za kulevya, huingia zaidi kutumia njia za bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na mipakani kwa njia ya magari binafsi au mabasi kupitia nchi za Kenya, Uganda na Mpaka wa Tunduma.

Ameyataja madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwamo kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi usioponyeka kirahisi na kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha matumizi ya dawa za kulevya. “Madhara ya kiuchumi ni pamoja na gharama kubwa za kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya, gharama kubwa za uchunguzi wa kimaabara kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na watumiaji wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia na kuendesha maisha yao,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote nchini zifanye maoteo na kuyawasilisha Bohari Kuu ya Dawa kabla au ifikapo tarehe 05 Machi 2017 ili kutekeleza azma ya Serikali ya kusambaza dawa kwa wakati.

“Dhamira ya Serikali ya kusambaza dawa kwa wakati kwenye Halmashauri zetu haitafanikiwa endapo Halmashauri zitachelewa kuwasilisha maoteo ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi. naomba kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge, mpate wasaa wa kufuatilia mchanganuo wa usambazaji dawa katika Halmashauri zenu ambao hutolewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,” amesema.

Amesema hali ya upatikanaji wa dawa nchini inaendelea kuimarika huku akitolea mfano kiasi cha sh. bilioni 91 ambacho kimeshatolewa, kati ya sh. bilioni 251 zilizotengwa sawa na wastani wa sh. bilioni 20 kwa mwezi.

Ili kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaatiba nchini, Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kununua madawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya mawakala.

“Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, utaratibu huo umeanza na tayari Serikali imekamilisha taratibu za kimkataba na wazalishaji watano wakubwa wa ndani ambao watanunua baadhi ya dawa kutoka ndani ya nchi, wakati mikataba mingine 76 ya wazalishaji wa nje iko katika hatua za mwisho. Matarajio yetu ni kwamba, utekelezaji wa mikataba ya nje utaanza katika mwaka wa fedha 2017/18,” amesema.

Amesema kutokana na uamuzi huo wa Serikali pamoja na jitihada za Serikali za kuongeza bajeti ya ununuzi wa dawa, Bohari ya Dawa imeweza kununua aina 105 za dawa muhimu sawa na asilimia 78 ya aina 135 ya dawa muhimu zinazohitajika nchini.

“Shabaha yetu ni kwamba, ifikapo Juni, 2017 usambazaji wa dawa muhimu nchini kote uwe umefikia asilimia 85. Taarifa hiyo imetolewa kwa kila Mheshimiwa Mbunge ili aweze kufuatilia kwa karibu dawa na vifaatiba vinavyoletwa na Serikali kwenye Halmashauri zenu,” amesema.

Bunge limeahirishwa hadi Jumanne, Aprili 4, 2017.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
IJUMAA, FEBRUARI 10, 2017
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: