Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam unayo furaha kuwa mwenyeji wa mwanamuziki maarufu wa Kimarekani wa miondoko ya ‘folk na blue grass’ Natalia Zukerman na kundi lake atakapokuwa katika ziara iliyosheheni ya Kimuziki kuanzia Februari 7- 12. Ziara ya Natalia na kundi lake nchini Tanzania ni mwanzo wa ziara yao ya nchi nne inayofadhiliwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani kama sehemu ya Programu ya kupeleka muziki wa Kimarekani katika mataifa ya nje. Nchi nyingine watakazotembelea ni pamoja na Zambia, Msumbiji, na Malawi.
Katika kuanza ziara yao, wasanii watatu wa kundi hili wataendesha kongamano katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Februari 8, wakishirikiana na wanamuziki kutoka Bagamoyo na vitongoji vyake. Kilele cha kongamano hilo jioni itakuwa ni burudani ya muziki, ambapo kutakuwa na onyesho la pamoja la muziki kati ya kundi la Zuckeman na washiriki wa kongamano.
Aidha, Zukerman na kundi lake wataendesha madarasa ya mafunzo maalum ya muziki kwa siku kadhaa katika kituo cha Music MayDay, kituo cha kwanza cha mafunzo ya muziki na dansi kisicho cha kiserikali jijini Dar es Salaam. Kundi hili litahitimisha ziara yake kwa burudani ya pamoja ya nguvu kwa wageni waalikwa katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Akiwa amekulia katika jiji la New York, Natalia Zukerman ni binti wa wanamuziki wa muziki wa kale wa kimagharibi (classical musicians) Eugenia and Pinchas Zukerman. Alisomea sanaa katika chuo cha Oberlin huko jimbo la Ohio na sasa anaishi Brooklyn, NY, ambako huandika, hucheza muziki na kuchora. Tangu mwaka 2001, Zukerman ametoa albamu sita studio na albamu moja ya iliyorekodiwa katika onyesho jukwaani aliyooiita Gypsies & Clowns.
Wasanii katika Programu ya kupeleka muziki wa Kimarekani katika mataifa ya nje (American Music Abroad) wanawawakilisha kizazi kipya cha mabalozi wa kimuziki, wanaowagusa watu si tu katika kumbi za burudani bali pia katika kushirikiana na wanamuziki na raia wa nchi nyingine duniani kote. Kila mwaka, karibu makundi kumi ya muziki wa asili ya Kimarekani wa aina tofauti huchaguliwa kushiriki katika ziara ya mwezi mmoja, katika nchi tofauti, ambapo hujumuika na halaiki za kimataifa katika burudani za hadhara, maonyesho ya pamoja na wanamuziki wa nchi hizo, mihadhara na maandamano, makongamano na mahojiano na vyombo vya habari. Bendi za American Music Abroad zimesafiri katika nchi zaidi ya 100 duniani kote toka mwaka 2011.
Toa Maoni Yako:
0 comments: