Wakati mahakama ikipanga kutoa uamuzi wa dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema) Desemba 14, 2016 Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Vicent Mashinji ametinga mahakamani hapo na kuitaka ijiamini na kutenda haki.

Lema alikamatwa na polisi akiwa Dodoma Novemba 2 na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchochezi.

Jana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilishindwa kusikiliza maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya kukata rufaa ya kupinga kuzuiwa kwa dhamana ya Lema.

Mawakili wa Serikali waliomba muda wa kuwasilisha hoja za kupinga maombi hayo.

Maombi hayo, yaliyotarajiwa kusikilizwa jana na Jaji Dk Modesta Opiyo yalikwama kutokana na kusudio la pingamizi lililowekwa na mawakili waandamizi wa Jamhuri katika shauri hilo, Paul Kadushi na Maternus Marandu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Jaji Opiyo kuahirisha kusikiliza maombi hayo, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema mawakili wa Serikali, wameomba wapewe muda kuwasilisha kiapo kinzani dhidi ya maombi hayo.

Alisema Jaji Opiyo alitumia busara kutoa uamuzi kuwa mawakili wa Jamhuri wawasilishe hoja hizo, Desemba 13 na upande wa utetezi utazijibu siku hiyo hiyo na uamuzi utatolewa Desemba 14, saa 6.00 mchana.

Mashinji atinga kumnusuru Lema

Akizungumza baada ya maamuzi hayo ya mahakama, Dkt. Mashinji alisema chama hicho kina imani kubwa na mahakama kuwa itatenda haki,.

Dkt. Mashinji ambaye alifika mahakama hapo kwa mara ya kwanza alisema kama wadau wa haki wamekuwa na ukakasi kwa jinsi suala la Lema linavyokwenda na inaonekana mahakama inalegalega.

“Tunaomba mahakama iendelee kujiamini ikijua ni mhimili unaojitegemea katika kutenda haki na impe haki yake ya dhamana Lema, kwa kuwa kosa analoshtakiwa lina dhamana na anajua katika uendeshaji wa masuala hayo kuna mambo ya kisiasa na utaalamu,”alisema.

Aliongeza kuwa inafahamika katika uendeshaji wa kesi kuna masuala ya kitaalamu na siasa, lakini kwa upande wa kesi ya Lema wanadhani kuna masuala ya kitaalamu zaidi.

“Lema ni kiongozi wetu, ni kiongozi wa kitaifa ni mbunge, mtu ambaye hatuna shaka ya kuwapo kwake kwenye jamii, anaweza kushughulikia suala hili na kujieleza akiwa nje,” alisema.

Dk Mashinji ambaye mapema juzi alimtembelea Lema gerezani Kisongo alisema ana imani kuwa mahakama itampa Lema haki yake.

Naye, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alitoa wito kwa vyombo vya dola kuacha kuwazuia wananchi wa Arusha kusikiliza shauri hilo.

Hata hivyo, jana Lema hakufika mahakamani, kwa kile kilichoelezwa kuchelewa kupelekewa hati ya kufikishwa mahakamani.

Lema anaendelea kushikiliwa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi wa hakimu mkazi, Desdery Kamugisha aliyempa dhamana Lema katika kesi namba 440 na 441/2016 ya kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.

Lema anatuhumiwa kuwa kati ya Oktoba 23 hadi 26, mwaka huu alitoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli katika maeneo tofauti katika mikutano yake ya hadhara.

Miongoni mwa kauli za Lema ni: “Nchi itaingia katika machafuko kama haitafuata misingi ya katiba na sheria na pia Rais Magufuli asipobadilika”

Lema pia akiwa katika uwanja wa shule ya Sekondari Baraa alitoa kauli kuwa: “Kiburi cha Rais akiendeea kujiona yeye ni Mungu, hatafika 2020, Mungu atakuwa amechukua maisha yake, Rais ni mbabe…”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: