Baadhi ya wanachama Wa (UVCCM) mkoa Wa Arusha wakiwa wanaminyana na askari Wa chama cha mapinduzi kuzuia kufunga ofisi hiyo kutokana na mgogoro uliopo Wa kutaka Katibu Wa zamani Ezekiel Molel alieamishwa kukabidhi ofisi kwa Katibu mpya.
Na Woinde Shizza, Arusha.

Baadhi ya vijana wa chama cha mapinduzi mkoa wa Arusha (UVCCM) leo wamefanya Vurugu katika jengo la makao makuu ya ofisi za jumuiya ya umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Arusha baada ya baadhi ya vijana wa umoja huo kufunga ofisi hizo

Tukio hilo lilitokea majira ya asubuhi ambapo baadhi ya vijana hao walijitokeza katika ofisi hizo na kufunga ofisi hizo na mara baada ya kufunga wakati walipoondoka ndipo mwenyekiti wa (UVCCM) Lengai Ole Sabaya akiwa na baadhi ya viongozi wa chama na vijana wa chama hicho kujitokeza na kisha kuzifungua kabla ya jeshi la polisi kuingilia kati.

Katika vurugu hizo jeshi la polisi mkoani Arusha linamshikilia mwenyekiti wa miradi ya jumuiya hiyo,Phillemon Amo ambapo alikamatwa na kisha kufikishwa mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati mkoani hapa.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya ofisi hizo kufungwa kwa minyororo jana majira ya saa 8;00 asubuhi na baadhi ya wanachama wa umoja huo wakipinga kitendo cha katibu aliyehamishwa, Ezekiel Mollel kuendelea kushikilia ofisi.

Hatahivyo,majira ya saa 11;30 kundi linguine la baadhi ya wanachama wa umoja huo likiongozwa na mwenyekiti wa jumuiya hiyo mkoani Arusha, Lengai Ole Sabaya lilifika na kisha kufungua tena ofisi hizo.

Mara baada ya tukio hilo ndipo jeshi la polisi mkoani hapa majira ya saa 11;00 asubuhi liliwasili katika ofisi hizo na kumshikilia mwenyekiti huyo na kisha kumfikisha mbele ya kituo kikuu cha polisi cha kati.

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Charles Mkumbo alithibitisha kushikiliwa kwa kiongozi huyo huku akisema kwamba atatoa taarifa kamili mara baada ya kumaliza mapokezi ya ugeni wa serikali mkoani hapa.

“Ni kweli tumemkamata lakini nina ugeni wa serikali naomba nitoe taarifa baadae”alisema Mkumbo lakini alipotafutwa baadae simu yake iliita bila kupokelewa

Awali baadhi ya wanachama wa umoja huo waliwasili majira ya asubuhi na kisha kufunga kwa minyororo ofisi hizo kwa madai ya kupinga kitendo cha katibu aliyehamishwa,Ezekiel Mollel kushindwa kukabidhi ofisi na kumpisha katibu mteule, Said Goha.

Wanachama hao waliwasili katika eneo hilo na kisha kufunga ofisi hizo huku wakimtaka Mollel akabidhi ofisi hiyo haraka kwa madai uhamisho wake ni utaratibu wa kawaida ndani ya jumuiya hiyo na unapaswa kuheshimiwa.

Hatahivyo,mara baada ya muda mchache kundi jingine la wafuasi wa umoja huo likiongozwa na Ole Sabaya liliwasili katika ofisi hizo wakiwa na nyundo,vyuma na mawe na kisha kuanza kukata minyororo iliyokuwepo na kufungua ofisi hizo.

Akizungumza mara baada ya kufungua ofisi hizo Ole Sabaya alisema kwamba yeye kama mwenyekiti anapinga vikali na kulaani kitendo cha baadhi ya wanachama wa umoja huo kufunga ofisi hizo kinyume na taratibu.

Mwenyekiti huyo alisema kwamba tayari wamevitaarifu vyombo vya dola kuchukua hatua na kuchunguza kwa kina tukio hilo kwa kuwa kufungwa kwa ofisi hizo anahisi ni njama za kutaka kuhujumu taasisi yao.

“Ofisi ni lazima zifunguliwe ili kazi za vijana ziendelee lakini tumevitaarifu vyombo vya dola kuanza kuchunguza kwa kina tukio hili kwa kuwa tunahisi hizi ni njama za kutaka kutuhujumu”alisema Ole Sabaya

Akizungumzia suala la Mollel kushindwa kukabidhi ofisi Ole Sabaya alisema kwamba katibu huyo hatakwenda popote kwa kuwa kuna njama zinasukwa kwa lengo la kupoteza ushahidi wa baadhi ya tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ndani ya umoja wao kwa kumwondoa katibu huyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: