Nianze kwa kumshukuru subh ana wa tala wabarakatu,(Allah) muuumba wa vitu vyote vinavyo onekana na visivyo onekana,nimefika siku ya leo tarehe 20-09-2016, kwa mapenzi yake tu, nikiwa bukheri wa Afya,nani washukuru wananchi wa Manispaa ya Kinondoni kwa kunipa ushirikiano na ulinzi wa nguvu ya umma wakati wote,nilitembea kifua mbele sikuwa na cha kuhofia.
Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa wafanyakazi wa Manispaa ya Kinondoni, mmenifanya mmenibadilisha fikra sana, kwa jinsi mlivyojitoa kuhudumia umma, wakati wote na kila mara kiongozi yeyote alipowatuma mlinyanyuka bila kujiuliza uliza hata pale ambapo majukumu yalipo wazidi kwa uzito na hamkuwahi kulalamika, hakika nyinyi ni nguzo msiyopaswa kudhalauliwa na kiongozi wa siasa yeyote yule, ukiondoa wachache wenye nia ovu ambao wanasiasa wengi wamewatumia hao kuadhibu wote.
Kutoka katika sakafu ya moyo wangu Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Madiwani Manispaa ya Kinondoni awamu ya tano, lenye wabunge wakuchaguliwa (J.J MNYIKA, H.Mdee. M.Mulia, S.Kubenea) na viti maalumu, wateule wa Rais na Madiwani wote, ushauri wenu na moyo wenu dhidi ya Halmashauri yetu ilinijenga na kuniimarisha, tulipingana kwa hoja hatukutenganishwa na itikadi, michango yenu pia ushauri wenu ulinifanya nionekane bora wakati wote ndani na nje ya Manispaa kama alama kuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Mwisho na kwa Umuhimu mkubwa niwashukuru sana waandishi wa habari, ambao ndiyo ubao wetu wa matangazo kuhusu umma wa wanakinondoni, ndiyo spika zetu zidi ya watu wetu, mmefikisha habari kwa wakati na nyinyi mlileta kero za Wananchi kwa weledi wenu, iwe kwa Magazeti, Televisheni, Radio, Blogs na Mitandao ya kijamii (social media) mliitendea haki Manispaa ya Kinondoni chini yangu sina cha kuwalipa ila mwenyezi Mungu kwa kuwa kila mtu na tunu yake amemuandalia malipo. Kwa unyenyekevu mkubwa ninaomba nifafanue kwa kuainisha baadhi ya mambo kama ifuatavyo:-
1. KUHUSU MGAWANYO WA HALMASHAURI YA KINONDONI NA UBUNGO.
Wilaya mpya ya ubungo ilipatikana mwishoni mwa kipindi cha awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho kikwete na GN (Government Notes) kusainiwa rasmi 25 Novemba 2015, Kwa wakati wote mpaka sasa tulishajua kuwa kuna wilaya mpya kilichokuwa kinasubiriwa ni taratibu za upatikanaji wa Halmashauri mpya ya Ubungo, lakini kuanzia Julai 2016, tumepata Mkurugenzi na Septemba Mosi 2016, watumishi zaidi ya 2,500 waligawanywa kwenye wilaya hizi mbili, na watumishi zaidi ya 1000 wakaripoti ofisi mpya za Halmshauri ya Ubungo tangu Septemba Mosi mwaka huu (2016) wakiwa wanaendelea na majukumu yao bila ya Baraza la Madiwani, tayari bajeti imeshagawanyika mara mbili ambao billioni 116 kwa halmashauri ya ubungo na billioni 126 kwa halmashauri ya Kinondoni, magari na vyanzo vya mapato ikiwemo uwekezaji vilishagawanywa siku nyingi, pamoja na usajili wa nembo ya Halmashauri ya Ubungo na akaunti zake za Benki.
2. MAFANIKIO KATIKA KIPINDI CHA UONGOZI.
Kipindi cha tangu January mpaka Agosti 2016, chini ya ukawa tumefanikiwa mambo mengi sana kwa uchache nitataja yafuatayo:-
(i). Kupandisha mapato ya halmashauri kutoka kuwa billioni 45, mwaka wa fedha 2015/ 2016 tuliyo ikuta mpaka billioni 67, 2016/2017 kwa Sasa.
Kwa kutumia Tafiti za kina tumeibua vyanzo vya mapato vya misingi vipya 7 na kuboresha vya zamani ili kupanua wigo wa kodi (tax base) na kuongeza makusanyo ya mapato yatokanayo na kodi.
(ii). Bajeti ya miradi ya maendeleo kupanda kutoka kuwa billioni 42.7 kwa mwaka 2015 /2016 mpaka billioni 110, kwa mwaka 2016/2017 huku billioni 40, nikutoka mapato ya ndani na billioni 50 ni kutoka Benki ya Dunia kupitia miradi ya DMDP, kilichobaki ni ruzuku kutoka Serikali Kuu LGDCG.
(iii). Uimarishaji wa Utawala Bora kwa posho za wenyeviti serikali za mitaa na wajumbe wake.
(iv). Kupambania mikopo ya Wanawake na Vijana kutoka kiasi cha sh millioni 200 tangu 2007 mpaka 2015 tuliyo ikuta katika Benki ya Wananchi ya Dar es Salaam (DCB) mpaka kufanikiwa kupandisha kuwa billioni 2.2 kwa kipindi cha miezi 7 tu.
( v). Huduma za uchocheaji wa miradi ya Maendeleo kama usimamiaji wa kugawa greda kwa wananchi, wao wakichangia mafuta tu.
(vi). Kupunguza kiwango cha utegemezi wa fedha za miradi ya maendeleo kutoka asilimia 80 ya utegemezi mpaka 61.3 ya utegemezi ambapo serikali kuu inatulipia mishahara na watumishi ni 90% miradi ya Maendeleo ni 15% na manispaa inalipa mishahara 15% na miradi ya Maendeleo inajitegemea kwa 85%.
( vii). Kupunguza na kubana mianya ya rushwa, kubebana na kutoa kazi kwa maagizo, ikiwemo kuzifuta kazi za viongozi waliopo juu serikalini waliopewa kazi kwa shinikizo la vimemo pasipo kuzingatia sifa stahiki za kitaaluma na kitaalam na michakato huru ya zabuni.
( viii). Migogoro ya ardhi na uuzwaji wa maeneo ya umma ikiwemo maeneo ya makaburi, huku migogoro ya ardhi ya Nyakasangwe, Kunduchi Meco na b kwa kushirikiana na wabunge, madiwani na taasisi zingine za umma.
(ix). Upunguzaji wa foleni, katika barabara za mitaa na zile kuu, kwa kupata ufadhili wa Benki ya Dunia tumeachia mchakato wa kupata mkandarasi wa kufungua, Msasani soko la samaki - Tanesco Mikocheni, MMK Mwananyamala, NZASA na Viwanadani.
(x). Miradi ya kuchakata taka ngumu ili kupunguza uchafu kwenye Manispaa yetu ya Kinondoni kwa ufadhili wa Wajerumani na huku Baraza limeridhia kulipa kodi ya milioni 900.
3. CHANGAMOTO KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI.
Katika kutekeleza miradi tumekumbana na vikwazo vingi kama ifuatavyo:-
(i). Kufanya kazi na wanasiasa wasiojua miiko ya uongozi na usimamiaji wa maslahi ya umma, kwa maana kwao waliona kama Manispaa ya Kinondoni ipo chini ya waasi badala ya kuona wapinzani ni njia mbadala ya maendeleo, kiasi cha kukwamisha miradi ya maendeleo, husuani viongozi wa kuteuliwa.
4. NAENDA UBUNGO, KUIJENGA UBUNGO YETU.
Natambua kuwa ipo fursa ya kung'ang'ania kuwa Meya Manispaa ya Kinondoni kwa mujibu wa sheria na mifano ipo, kuwa meya ni wa miaka 5, siyo miezi 7, ila sina sababu ya kung'ang'ania kubaki Kinondoni hata kama fursa hii ipo, kwakuwa kata yangu nilikopewa ridhaa na wanachi ni kata ya UBUNGO, ipo jimbo la UBUNGO wilaya ya UBUNGO, kubakia Kinondoni inaweza kutafsiriwa ni kuwasaliti wananchi wangu wa Ubungo.
Sio hilo tu pia, wilaya hii nilikuwa muasisi wa mapambano ya kuiomba serikali itupatie WILAYA harakati zilizo asisiwa na Mhe. JOHN JOHN MNYIKA, na mimi nikiwa diwani 2010-2015, na kwanba tulikuwa na sababu ya kuomba wilaya tofauti na CCM walikuwa wakiomba majimbo, tuliamini kuwa wananchi waliokuwa milioni 1.1 jimbo la Ubungo (zamani) walikuwa wanahitaji sana huduma za idara ya afya, ardhi, maji, biashara na muindombinu ili kuondokana na ubabe wa PETTY CLASS OR BOURGEOSIE walioamini kuwa huduma bora ziende kwao UZUNGUNI, na watu wa Manzese Kimara na Goba wawe na jukumu la kuchangia mapato tu.
Leo Wananchi wa UBUNGO watakuwa na fursa ya kujichagulia maendeleo yao ya bilioni 116, ndiyo maana najiona mzalendo kwa kusema naenda NYUMBANI, naenda UBUNGO, naenda HOME SWEAT HOME. kuijenga Ubungo yetu mpya kwa moyo na uzalendo chini ya utumishi uliotukuka kama chama kitaendelea kunipa ridhaa, mkazo na msisitizo.
Katika kuifanya Ubungo kuwa ya kisasa na ufanisi makini tutaanza na vipaumbele vifuatavyo:-
1. KUPANGA UBUNGO (MIPANGO MIJI).
2. KUKUSANYA MAPATO YA NDANI(OWN SOURCE).
3. KUJAZA MORALI WATUMISHI NA VIONGOZI.
4. MIUNDOMBINU (BARABARABARA NA MITARO).
5. USAMBAZAJI WA HUDUMA ZA KIJAMII, ELIMU, AFYA, MAJI, NA KILIMO NA UFUGAJI.
5. UCHAGUZI WA MEYA KINONDONI NA UBUNGO.
Ni dhairi shahiri kuwa Manispaa hizi zitendelea kuwa chini ya UKAWA, na siyo kwa mapenzi binafsi niliyo nayo ila wazungu wanasema "Numbers don't lie" kwa kauli hiyo Manispaa ya Temeke inagawanywa kuwa Kigamboni na Temeke, ni dhahiri zote mbili zitaendelea kuwa chini ya CCM, kwakuwa namba hazipo kwenye mapenzi binafsi, ila ukweli CCM wamezidi namba dhidi ya UKAWA. Kiuhalisia na ukweli katika mgawanyo wa Halmashauri zote mbili upo hivi kama ifuatavyo:-
A. HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO.
Katika Manispaa ya Ubungo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kina viti vya Madiwani 10 na Idadi ya wabunge wa Majimbo (Ubungo na Kibamba) 2, Chama Cha Wananchi (CUF) kina viti vya Madiwani 2, na Chama Cha Mapinduzi(CCM) kina viti vya Madiwani 2 na Madiwani wa Viti Maalum 2.
Ukiachilia mbali CCM, CHADEMA na CUF katika Halmashauri ya Ubungo havina Madiwani wa viti Maalumu. Kwa hesabu hizo hapo juu katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, CHADEMA inajumla ya Madiwani 10 na wabunge 2 hivyo Jumla kuwa 12, na CUF Madiwani 2,
Hivyo kufanya UKAWA kuwa na idadi ya Madiwani 14. Na CCM kuwa na Jumla ya Madiwani 4. Hivyo ni wazi kwamba UKAWA wataongoza Manispaa ya Ubungo.
B. HALMASHAURI YA MANISPAA YA KINONDONI.
Katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kina viti vya Madiwani 8 (Kawe 5 na Kinondoni 3), wabunge wa Jimbo 1(kawe), Madiwani wa viti maalum 7, na Chama Cha Wananchi (CUF) kina viti 3, Madiwani Viti Maalum 2 na Mbunge wa Jimbo 1 (Kinondoni) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina viti 9 (Kawe 5 na Kinondoni 4), Madiwani wa viti maalum 2 wateule wa Rais 3 na wabunge wa vitu maalum 2.
Kwa hiyo CHADEMA ina viti vya Madiwani 17 na CUF ina viti 7 na CCM ina viti 16, hivyo haihitaji miujiza kujua kuwa kwamba Halmashauri ya Kinondoni itaongozwa na UKAWA. Hii itakuwa na maana;-
UKAWA 24
CCM 16
MWISHO
Nipo njiani naelekea kwenye mkutano wa Mameya wote, unaofanyika Musoma mkoani Mara kupitia Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) tarehe 22 - 24 Septemba, kumalizia majukumu yangu rasmi kama Meya wa Manispaa ya Kinondoni, na kufanikiwa kuingia rasmi kwenye orodha ya kuwa meya wa tatu (3) tangu Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuanzishwa 1. SALUM LONDA 2. YUSUPH MWENDA 3. Boniface Jacob B.
Kwa unyenyekevu mkubwa naomba wananchi wa Kinondoni kunipigia kura ya kuwa Meya bora, zikiwa zimebakia siku mbili kuhitimisha hilo, kama njia ya kuienzi Kinondoni yetu. Aksanteni kwa ushirikiano wenu. #tukutaneubungo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: