Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, (katikati) akiwatoka mabeki wa Ndanda FC wakati wa mchezo wao wa ligi Kuu Tanzania bara uliofanyika katika Uwanaja wa Taifa Dar es Salaam jana Simba ilishinda mabao, 3-1.
Mshambuliaji wa Simba,Laudit Mavugo akipiga kichwa mpira huku akizongwa na mabeki wa Ndanda FC wakati wa mchezo wao wa ligi Kuu Tanzania bara uliofanyika katika Uwanaja wa Taifa Dar es Salaam jana Simba ilishinda mabao, 3-1.
SIMBA SC imeanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kishindo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Japokuwa hakufunga hata bao moja, lakini beki wa kulia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye anastahili sifa zaidi kwa ushindi mnono wa Simba leo, kutokana na kuseti mabao yote.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Simba SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji kutoka Burundi, Laaudit Mavugo dakika ya 20 aliyemalizia mpira wa adhabu wa Tshabalala.
Mshambuliaji anayeinukia vizuri nchini, Omary Mponda akaisawazishia Ndanda FC dakika ya 37 kwa kichwa akimalizia krosi ya Nahodha Kiggi Makassy.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog kipindi cha pili akiwatoa Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib na kuwaingiza Mwinyi Kazimoto na Frederick Blagnon yaliiongezea uhai Simba na kuvuna mabao zaidi.
Mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Blagnon alianza kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 73 kwa kichwa akimalizia kona ya Tshabalala.
Nyota wa mchezo wa leo, Tshabalala akaseti bao la tatu baada ya kupiga kona iliyotemwa na kipa Jackson Chove na winga Shizza Ramadhani Kichuya akasukumia nyavuni kuipa Simba SC ushindi wa 3-1.
Kwa ujumla Simba SC imecheza leo na ilistahili ushindi huo, wakati Ndanda walionyesha upinzani kwa wenyeji kipindi cha kwanza pekee.
---
MATOKEO KATIKA VIWANJA VINGINE:
Azam Fc 1- African Lyon 1
Mtibwa Sugar 0- Ruvu Shooting 1
Stand United 0- Mbao Fc 0
Maji maji 0- Tanzania Prisons 1


Toa Maoni Yako:
0 comments: