Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na Waandishi wa Habari pamoja na baadhi ya Maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) juu Maadhimisho ya kilele cha miaka 52 ya jeshi hilo.
Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), Kanali Ngemela Lubinga (aliyesimama) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kazi mbalimbali watakazozifanya katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi hilo.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akisalimiana namakamanda wa Jeshi la Ulinzila Wananchi wa Tanzania JWTZ, alipokutana nao ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Agosti 30, 2016. JWTZ itaadhimisha miaka 52 kwa kufanya usafi kote nchini.
Na Bakari Issa Madjeshi, Globu ya Jamii
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania JWTZ linatarajia kuadhimisha siku ya kilele cha miaka 52 tangu kuzaliwa kwake kwa kufanya usafi wa mazingira sambamba na uchangiaji wa damu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipokutana na Maafisa wa Jeshi hilo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema JWTZ inapotimiza miaka 52 ni fahari kubwa hivyo tunapaswa kuwapongeza kwa kudumisha amani na mshikamano,kusaidia mataifa mbalimbali pamoja na kulinda mipaka ya nchi.
Makonda amesema kuwa Wananchi wanapaswa kuungana nao katika kazi mbalimbali wanazofanya katika mkoa wa Dar es Salaam.
"Wakuu wa Wilaya wamejipanga kuainisha maeneo ambayo yatafanyiwa usafi hivyo kama kuna mwananchi anataka kushiriki nao usafi na Wanajeshi siku ya kilele, Septemba mosi basi asubuhi na mapema waripoti kwa Wakuu hao wa Wilaya na watapangiwa jinsi gani wataweza kushirikiana nao"amesema Makonda.
" Pia wamekubali kuchangia Damu hii itasaidia kutokana na mahitaji ya Damu ni makubwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na pia hospitali za Mwananyamala, Temeke na Amana"ameeleza Mkuu wa Mkoa huyo wa Dar
Pia ametoa wito kwa wananchi wapenda amani kujitokeza kwa wingi kuchangia damu katika maeneo ya Lugalo, JKT Kawe na maeneo mengine ya kambi yenye vituo vya uchangiaji damu.
Akithibitisha kuwepo kwa Maadhimisho ya kilele cha miaka 52 ya JWTZ, Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Ngemela Lubinga amesema Mkuu wa Majeshi amefarijika kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kuadhimisha miaka 52 ya Jeshi hilo.
Kanali Lubinga amesema wamefarijika kuona Mkoa wa Dar es Salaam umeshiriki nao katika shughuli mbalimbali za Jeshi hilo ikiwemo shughuli za usafi.
"Siku hiyo ya kilele shughuli zetu zitakuwa ni utoaji damu, kufanya usafi kutokana na usafi ni afya na ni amani" amesema Kanali Lubinga
Amesema kutakuwa na Madaktari wa Jeshi watakao toa huduma za ushauri kwa magonjwa mbalimbali kama Kisukari pamoja na Shinikizo la Damu sambamba na kushiriki Michezo.
Pia amesema Ndege za kivita zitakuwa zitapita kuashiria siku ya kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: