Timu ya Jamii Media ikitambulishwa mbele ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Bukoba.

Meya wa Manisapaa ya Bukoba, Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini na Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media wakisaini makubaliano ya kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa Tushirikishane.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Bw. Maxence Melo akimkabidhi kitendea kazi mwakilishi wa JamiiForums (Afisa Mawasiliano) katika Jimbo la Bukoba Mjini, Bi. Happiness Essau.
Mkufunzi akitoa maelezo juu ya matumizi sahihi ya mtandao wa JamiiForums.
Mbunge wa Bukoba Mjini, Mhe. Wilfred Lwakatare akijibu baadhi ya maswali na kutolea ufafanuzi hoja zilizotoka kwa wapiga kura.
Diwani wa Kata ya Bakoba, Mhe. Mwakyoma akiwasilisha kundi lake juu ya Wajibu wa Mbunge kwa wapiga kura wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media Mhe. Maxence Melo akibadilishana mawazo na waheshimiwa madiwani Kalumuna(katikati) ambaye ni diwani wa Bilele(CCM) na Kabaju (kulia) ambaye ni diwani wa Kashai (CHADEMA).
Mbunge wa Bukoba Mjini, akishirikiana na wapigakura wa Jimbo lake katika zoezi la kuchambua kazi na wajibu wa mbunge kwa wapiga kura wake.
Washiriki wa Warsha ya Tushirikishane katika Jimbo la Bukoba Mjini wakiwa katika picha ya pamoja.

Baraza la Halmashauri ya Bukoba, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Pamoja na Timu ya Jamii Media katika picha ya Pamoja.
---
Mtandao wa JamiiForums.com umezindua rasmi mradi wa unaowashirikisha
viongozi wa kuchaguliwa(hususani wabunge na madiwani), Serikali
(Halmashauri) na Wananchi katika kurahisisha upatikanaji wa maendeleo.
Mradi
huu unaotambulika kama "Tushirikishane" una malengo ya kuwawezesha
wabunge wa kuchaguliwa kutekeleza ahadi walizotoa wakati wa uchaguzi kwa
urahisi.
Pia Tushirikishane inalenga kuzisaidia
Halmashauri kuboresha utoaji huduma za jamii kwa ufanisi zaidi.
Mwitikio(maoni, ushauri na kero) wa wananchi katika mnakasha wa
Jimbo/Halmashauri utachukuliwa kwa umakini na viongozi hawa ili
kuhakikisha mrejesho unatolewa kwa wananchi.
Akizungumza
mbele ya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba Mjini, Mkurugenzi
Mtendaji wa Jamii Media na Mwanzilishi-Mwenza wa mtandao wa
JamiiForums.com, Bwana Maxence Melo aliwapongeza viongozi wa Wilaya,
watendaji wa Halmashauri, Madiwani na Mbunge kwa mwitikio mkubwa
walioonyesha katika kuupokea mradi wa Tushirikishane.
Maxence
aliwafahamisha kwamba Mradi huu utatekelezwa katika majimbo sita (6)
kwa kuanzia na Bukoba Mjini limekuwa Jimbo la kwanza katika kuanza
utekelezaji wake. Alifafanua kuwa mradi huu utachukua miezi 9 na hivyo
Wabunge wanaohusika kwenye mradi huu wanatakiwa kukubaliana na wananchi
juu ya ahadi zisizozidi 4 za kuweza kuwa sehemu ya mradi huu zinazoweza
kutekelezeka kwa kiwango kikubwa wakati wa mradi huo.
Bwana
Maxence pamoja na timu yake ya wataalam walikuwa Bukoba Mjini kwa siku
tano kuendesha warsha iliyowawezesha wadau kuuelewa mradi kwa ufasaha,
kutambua majukumu yao na kujua njia zitakazotumika katika kutekeleza
mradi kwa faida yao.
Warsha ya Tushirikishane
ilifanyika Bukoba Hotel na wadau wanaowakilisha Halmashauri ya Manispaa
ya Bukoba, Wapiga kura na wananchi wa Bukoba Mjini, Madiwani wa vyama
vyote pamoja na Mbunge wa Jimbo walishiriki.
Malengo ya Tushirikishane
Pamoja na lengo kuu tajwa hapo juu, Mradi huu una malengo mahususi yafuatayo:
i.
Kupanua wigo wa mawasiliano kati ya Wananchi na viongozi wa kuchaguliwa
na serikali yao (kwa njia ya mtandao, magazeti, redio, televisheni na
mikutano ya wazi)
ii. Kurahisisha upatikanaji wa habari na taarifa za umma zikiwa kwenye lugha rahisi
iii. Kuchochea majadiliano ya wazi, yenye tija na staha kati ya wananchi na viongozi wao
iv. Kusaidiana na viongozi wa kuchaguliwa katika kutengeneza nyenzo za muhimu katika kutekeleza ahadi.
Matarajio ya Mradi.
Shughuli
za Mradi huu zinatarajia kuchangia katika mabadiliko ya muda mfupi na
muda mrefu kwenye tasnia ya uongozi wa Uwakilisha nchini Tanzania.
Miongoni mwa matarajio hayo ni:
i. Kujengeka kwa utamaduni wa majadiliano yenye staha kati ya viongozi na wananchi kwenye mitandao ya kijamii
ii. Kuboreshwa kwa mfumo wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika utekelezaji wa sera na ahadi za wakati wa Uchaguzi.
iii. Kuongezeka kwa ufanisi katika utekelezaji wa sera na ahadi za kipindi cha uchaguzi.
Kufuatilia mradi huu, tembelea JamiiForums ( http://www.jamiiforums.com/threads/jamiiforums-yazindua-rasmi-mradi-wa-tushirikishane.1094133/ )


Toa Maoni Yako:
0 comments: