RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kutumia vizuri mitandao ili kulinda utamaduni pamoja na kuacha kuiga mambo yasiyopendeza wanayoyaona kutoka kwa wageni, televisheni na vyombo vengine vya habari ambayo ni kinyume na maadili na utamaduni wa Mzanzibari.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed, huko Michenzani katika uwanja wa Mnara wa Kumbukumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uzinduzi wa Tamasha la 21 la Utamaduni wa Mzanzibari.
Katika hotuba hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika karne hii tamaduni nyingi zimekuwa zikiathirika na nyengine kupotea kutokana na utandawazi pamoja na maendeleo ya teknolojia.
Alisema kuwa wapo wanaosema kuwa sasa ulimwengu umekuwa ni kijiji kwa hivyo wananchi wa Zanzibar ni lazima wahakikishe kuwa utamaduni wao hauathiriki kwa kuiga tamaduni mpya za kijiji hicho wasichokijua.
“Tuwe makini na tutambue kuwa kuna makundi kadhaa duniani yenye dhamira ya dhati ya kuharibu tamaduni na silka za watu mbali mbali, na kulazimisha watu wafuate, waige na wahusudu tamaduni zao”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kulinda utamaduni wa Mzanzibari, Serikali imekuwa ikihimiza matumizi mazuri ya teknolojia kwa upana wake na hasa matumizi ya mitandao ambapo kwa upande wake amekuwa akiendeleza na kusimamia jitihada zenye kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na matumizi mazuri ya mitandao kwa lengo la kulinda utamaduni wake.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa matamasha ya utamaduni yanayoendelea kufanywa mijini na vijijini ni muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho ikizingatiwa kuwa matamasha hayo yanatoa fursa ya kukumbuka na kufahamu mambo mbali mbali yaliyokuwa yakifanywa na wazee.
Vile vile, Dk. Shein alisema kuwa kupitia matamasha hayo jamii inaweza kufahamu historia ya Mzanzibari kwa namna mbali mbali kwani ni ukumbusho muhimu wa namna ambavyo wazee walivyokuwa wakiendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na michezo ya asili, kazi za mikono, kukuna nazi, kusuka ukili pamoja na mapishi mbali mbali.
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na waandalizi wa Tamasha hilo la 21 la utamaduni wa Mzanzibari kwa kauli mbiu ya “Dumisha Utamaduni na Amani, Piga Vita Udhalilishaji”, ambayo itazidi kutoa msukumo na kuhamasisha mashirikiano na ari ya kupambana na kadhia hiyo.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kulipuuza kundi la watu wachache linalopita likihubiri chuki, mgawanyiko na kuhamasisha roho mbaya katika jamii.
Alisema kuwa ni aibu kuona kwamba katika karne hii kuna watu miongoni mwa wananchi wanaendelea kuwashawishi wananchi wa Zanzibar kugomeana katika shughuli za mazishi na matanga na nyumba za ibada ili kukidhi matakwa yao binabsi.
Pia, Dk. Shein alitoa pongezi maalum kwa waandalizi wa sherehe hizo kwa kulitekeleza agizo lake alilolitoa mwaka jana la kuwashirikisha ipasavyo wajasiriamali katika Tamasha hilo kwani kazi za ujasiriamali zina umuhimu wa pekee katika kurithisha utamaduni wa Mzanzibari kutoka kizazi kimoja kwenda chengine.
Akitoa nasaha zake kwa suala hilo, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo kuendelea kushirikiana na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wazee, Vijana Wanawake na Watoto kwa lengo la kuwapa fursa zaidi wajasiriamali wa Zanzibar kuuza na kuonesha bidhaa mbali mbali wanazozitengeneza.
Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa ni umuhimu ikiwa kila wanapokutana katika mihadhara kama hiyo kukumbushana umuhimu wa kuimarisha usafi wa mazingira ili kuweza kuzuwia maambukizo ya maradhi ya kipindupindu.
Alisema kuwa Serikali huwa haipendi kuzuwia biashara za vyakula na vinywaji zinazofanywa na wajasiriamali na wafanya biashara ndogo ndogo kwani ndio wanaoathirika zaidi lakini hulazimika kuanya hivyo ili kunusuru maisha yao pamoja na wananchi walio wengi.
“Napenda kutoa shukurani maalum kwa wajasiriamali na wananchi wote kwa subira na mashirikiano wanayoendelea kuyatoa katika kupambana na maradhi ya kipindupindu”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa wazee na walimu wana jukumu la kufundisha watoto mila na desturi za Kizanzibari ikiwa ni pamoja na kuwafundisha na kuwahimiza kucheza michezo ya asili ili nao waje kuwa walimu kwa kizazi kijacho.
Dk. Shein aliihimiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kutilia mkazo suala la utamaduni kwenye mitaala ya masomo katika ngazi mbali mbali.
Nao uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ulieleza umuhimu wa Tamasha hilo huku ukisisitiza dhana nzima ya kauli mbiu ya tamasha hilo mwaka huu kwa jamii ya Kizanzibari.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma alisema kuwa udhalilishaji wa wanawake na watoto si utamaduni wa Zanzibar na ndio maana juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na Serikali kwani kuwafanyia hivyo ni vitendo vya kinyama.
Mapama Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Omar Hassan nae kwa upande wake alisisitiza haja ya kutumia fani za sanaa zilizopo hapa Zanzibar katika kuhakikisha zinatoa elimu kwa jamii yenye lengo la kuyatekeleza kwa vitendo yale yote yaliomo katika kaulimbiu ya mwaka huu ya tamasha hilo huku wakitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa mashirikiano makubwa aliyowapa.
Katika uzinduzi huo mapema mgeni rasmi alikagua kazi mbali mbali zinazofanywa na wajasiriamali waliofika katika uzinduzi huo na kupata nafasi kuwasikiliza mafanikio yao pamoja na changamoto zinazowakabili.
Burudani za aina mbali mbali zilikuwepo katika uzinduzi huo ikiwa ni pamoja na utenzi, ngoma za utamaduni pamoja na maonyesho ya mavazi ya utamaduni wa Mzanzibari.
Kila mwaka tamasha hilo limekuwa likiadhimishwa kwa mitindo na vionjo tofauti tokea lilipoanzishwa mwaka 1994 ambapo kwa mwaka huu sherehe za tamasha hilo zimezinduliwa hivi leo na zitadumu hadi Julai 25 mwaka huu litakapofungwa huko katika viwanja vya skuli ya Fukuchani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Toa Maoni Yako:
0 comments: