Mpigachapa Mkuu wa Serikali Bw.Cassian Chibogoyo akizungumza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa mkutano na waandishi hao katika kueleza jamii umuhimu wa kuzingatia matumizi sahihi ya vielelezo vya Taifa walipokutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi hiyo Julai 27, 2016 kulia kwake ni Afisa Habari Ofisi ya Waziri Mkuu Bi.Nyamagory Omary.
Mpigachapa Mkuu wa Serikali Bw. Cassian Chibogoyo akiwaonesha wanahabari (hawapo pichani) muonekano sahihi wa Nembo ya Taifa wakati wa mkutano wake na wanahabari Juali 27, 2016, wa kwanza kulia ni Afisa Habari Idara ya Habari Maelezo Bw. Frank Shijja.
Mpigachapa Mkuu wa Serikali Bw.Cassian Chibogoyo akionesha baadhi ya Vielelezo muhimu vya Taifa wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa ofisi yake Julai 27, 2016.
---
Mpigachapa Mkuu wa Serikali Ofisi ya Waziri Mkuu Bw.Cassian Chibogoyo amewataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya vielelezo vya Taifa kama njia ya kuheshimu Taifa na kuonesha uzalendo.
Chibogoyo ameyasema hayo hii leo katika kipindi cha pili cha ‘TUJITAMBUE’ ambacho kimewakutanisha waandishi mbalimbali wa vyombo vya habari Jijini Dar es salaam kwa lengo la kutoa muendelezo wa elimu sahihi ya vielelezo vya taifa kwa jamii.
Akitaja alama tatu muhimu za Taifa ambazo ni Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Ngao ya Taifa, Chibogoyo amesema kila kimoja kinasimamiwa na sheria ili kuhakikisha matumizi yake yanaliletea heshima Taifa la Tanzania hivyo, wananchi ni vyema wakawa sehemu ya kutunza tunu hizo na kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi.
Katika ufafanuzi wake ameeleza kuwa, Wimbo wa taifa una Tone Maalum na maneno maalum yaliyowekwa hivyo uimbaji unaoongeza vibwagizo kinyume cha uhalisia wake ni kosa kisheria.
Akielezea matumizi ya Bendera ya Taifa amesema ni kinyume cha sheria kubadili rangi zilizoainishwa kisheria kwani kila rangi ina maana yake na kuwa matumizi ya bendera serikalini yana utaratibu maalum kuanzia Ofisi ya Rais hadi kwa viongozi wa ngazi za chini.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pekee ndiye anayeweza kufanya mabadiliko ya Bendera ya Taifa na Ngao ya Taifa kama kinavyoagiza kifungu cha 5 cha sheria ya vielelezo vya Taifa Na. 15 ya mwaka 1971.” Alisema Chibogoyo.
Kuhusu Nembo ya Taifa amesema ziko nembo nyingi feki mtaani ambazo pia zinatumiwa na wananchi katika matangazo au shughuli za kibiashara kinyume na matakwa ya sheria huku akitumia kipindi hicho kuonesha tofauti zilizopo katika alama sahihi na zile ambazo si, sahihi.
Bwana Chibogoyo alihitimisha kikao hicho kwa kuwashukuru wadau wote na kusema kuwa tarehe ya kikao kingine itatolewa kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Waziri Mkuu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: