Wakili Jumaa Mhina 'Pijei' (wa kwanza kulia mbele), akila kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
Wakili Jumaa Mhina 'Pijei' (wa kwanza kulia), akisaini kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam.
---
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Wakili Jumaa Mhina 'Pijei', baada ya kula kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam juzi, amesema kazi kubwa iliyo mbele yake ni kuhakikisha anatatua kero mbalimbali za wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza katika viwanja vya Ikulu baada ya kula kiapo, Pijei, akiwa na wakurugenzi wenzake, alisema kuwa, kwa kushirikiana na viongozi wenzake wa wilaya hiyo akiwemo Mkuu wa wilaya, Daniel Chongolo na Ofisa Tawala wa wilaya watatekeleza majukumu yao ipasavyo.
"Ninaamini kwa kushirikiana na viongozi wenzangu walioteuliwa hivi karibuni, tutajitahidi kutatua kero za wananchi wetu," alisema.
Pijei alisema kuwa, uamuzi wa Rais John Magufuli kumteua kuwa mkurugenzi wa wilaya hiyo, umempe nguvu na kujiamini kuwa, hatamwangusha Rais Magufuli na wakazi wa wilaya hiyo.
Alisema licha ya wilaya hiyo kukabiliwa na changamoto nyingi atahakikisha wanatumia fursa mbalimbali kutatua kero hizo wakati wowote.
Wakili huyo alisema kuwa, pia atashirikiana na wenzake kuhakikisha wanaibua miradi mbalimbali itakayowainua kimapato vijana na akina mama wa wilaya hiyo.
"Hii wilaya iko mpakani na Kenya, hivyo tutatumia fursa zilizopo kwa kushirikiana na wananchi kuanzisha miradi itakayowainua kiuchumi, naamini Longido ina wananchi waelewa na wapenda maendeleo," alisema.
Alisema mara baada ya kuripo katika kituo chake cha kazi, atapata sehemu ya kuanzia kwani atakuwa amepata ripoti kamili ya wilaya hiyo na hata kutembelea sehemu mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments: