Hapa ni katika ukumbi wa mikutano wa mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama Mkoani Shinyanga.Kulia ni makamu wa rais wa Kampuni ya Uchimbaji ya dhahabu ya Acacia Deo Mwanyika akikabidhi jezi kwa rais wa Chama Cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) Godfrey Jax Mhagama kwa ajili ya mashindano ya mbio za baiskeli Kanda ya Ziwa Victoria yatakayofanyika siku ya Jumamosi, Julai 16,2016-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog.

Angalia Umbali wa njia na zawadi watakazopata washiriki wa shindano hilo siku ya Jumamosi,Julai 16,2016
Katikati ni makamu wa rais wa Kampuni ya Uchimbaji ya dhahabu ya Acacia Deo Mwanyika akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa ajili ya waendesha baiskeli watakaoshiriki katika shindano la mbio za baiskeli kanda ya ziwa siku ya Jumamosi Julai 16,2016.
---
Mashindano ya mbio za baiskeli kanda ya Ziwa yaliyondaliwa na Chama cha baiskeli Tanzania(CHABATA) yanayodhaminiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Acacia inayomiliki migodi ya Buzwagi,Bulyanhulu na North Mara yanatarajiwa kutimua vumbi Julai 16,2016 mkoani Shinyanga.

Mashindano hayo ya kusaka bingwa wa mbio za baiskeli kwa upande wa wanaume na wanawake kanda ya ziwa yanajumuisha washiriki 120 kutoka mikoa sita ya kanda ya ziwa ambapo kila mkoa utatoa washiriki 20.

Akizungumza leo wakati wa kukabidhi vifaa vya michezo kwa uongozi wa CHABATA kwa ajili ya mashindano hayo,Makamu wa rais wa Kampuni ya Acacia Deo Mwanyika alisema mashindano hayo yatakuwa katika makundi matatu,ambapo kundi la kwanza ni la wanaume, pili wanawake na kundi la tatu ni wafanyakazi wa migodi ya Acacia ambao nao watashiriki katika kundi lao.

Alisema ni mwaka wa tatu sasa Acacia imekuwa ikishirikiana na CHABATA kuendesha mashindano ya mbio za baiskeli kanda ya ziwa yenye mikoa sita ambayo ni Shinyanga,Mwanza,Geita,Simiyu,Mara na Kagera.

“Kampuni ya Acacia inajali wananchi katika maeneo mbalimbali,na kwenye eneo hili la michezo ufadhili wetu umekuwa mkubwa ambapo kila mwaka huwa tunatoa kiasi cha shilingi milioni 130 kusaidia kuendesha mashindano haya…tunafurahi kuwa mashindano haya kila mwaka yamekuwa ni mazuri na yanapendwa sana na wananchi wa kanda ya ziwa”,alieleza Mwanyika.

“Tangu tulivyoanza mwaka 2013 tumekuwa tukijitahidi kuboresha mashindano haya,tumekuwa tukitoa zawadi nyingi na nzuri lengo kubwa ni kuinua vipaji kwenye maeneo yanayotuzunguka ndiyo maana tumewapa kipaumbele wakazi wa maeneo haya”,aliongeza.

Mwanyika alisema kilele cha mashindano hayo kimekuwa kikifanyika Kahama kwa sababu kuna migodi miwili na kwamba hata mwaka huu yatafanyika wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Alieleza kuwa mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume ataondoka na kitita cha shilingi milioni 1,500,000/= ,kombe na medali na upande wa wanawake mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha shilingi 1,200,000/= ,kombe na medali.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa kwa ajili ya mashindano ya mbio hizo,Rais wa Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA) Godfrey Jax Mhagama,alisema wanaume wataendesha baiskeli kwa umbali wa kilomita 156.5 na wanawake wataendesha baiskeli kwa umbali wa kilomita 80.

Alieleza kuwa mbio za baiskeli kwa upande wa wanaume zitaanzia eneo la Maegesho ya Magari Makubwa lililopo Nyasubi mjini Kahama kuelekea Tinde na kurudi tena Kahama na wanawake wataanzia eneo la Maegesho ya Magari Makubwa kwenda Sungamile na kurudi tena Mjini Kahama.

Aidha Mhagama aliipongeza kampuni ya ACACIA kwa kuendelea kudhamini mashindano ya mbio za baiskeli hivyo kuwaomba wadau wengine wa michezo kujitokeza kuwadhamini kwani mchezo huo pamoja na kwamba unapendwa na watu wengi lakini una wadhamini wachache.

“Acacia imetusaidia kwa kiwango kikubwa katika mashindano haya, kwa kweli wametufundisha mahusiano mazuri na utendaji wa kazi…nje ya mashindano ya kanda ya ziwa pia mwaka 2015 walitusaidia kupeleka timu yetu ya taifa kwenye mashindano ya Afrika kule Afrika Kusini”,alieleza Mhagama.

“Tangu tuanze kupeleka wachezaji katika mashindano ya kimataifa,timu ya Tanzania haijawahi kupeleka wachezaji 9 kwa mkupuo mmoja,lakini kwa msaada wa Acacia tumeweza,na kwa mara ya kwanza Tanzania imepeleka wachezaji wa kike kwenye ubingwa wa Afrika kwa msaada wa Acacia”,aliongeza Mhagama.

Alisema mwaka jana wachezaji wote 200 walioshiriki mbio za baiskeli kanda ya ziwa walivalishwa jezi za baiskeli na kufanikiwa kupata mabingwa wa kanda ya ziwa wanaowakilisha nchi katika michezo mbalimbali.

“Tangu tuanze mashindano haya,tumekuwa na idadi kubwa ya wachezaji kutoka kanda ya ziwa wanaochaguliwa kujiunga na timu ya taifa”,alisema Mhagama.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: