Mhe.Pinda akisisitiza jambo (Picha zote na Naamala Samson).
Bw.Maganga akielezea historia fupi ya GO BIG MOVEMENT mbele ya Mhe. Pinda.
 Vijana wa Go Big Movement wakitazama ng’ombe kijijini Zuzu kwa Mhe. Pinda.
---
Na Naamala Samson

Aliyekuwa waziri mkuu wa serikali ya awamu ya nne, Mhe. Mizengo Pinda, amewahimiza vijana wa kitanzania kujishughulisha na kilimo na ufugaji wa kisasa ili kupata matokeo bora na kuinua kipato chao na cha taifa kwa ujumla.

Mhe.Pinda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki shambani kwake katika kijiji cha Zuzu mkoani Dodoma alipotembelewa na umoja wa wajasiriamali vijana wa GO BIG MOVEMENT wapatao arobaini na mbili(42) waliokuwa katika ziara ya kujifunza kwa vitendo kuhusu ukulima na ufugaji wa kisasa. Aliwahimiza vijana hao kutokata tamaa pindi wanapopata changamoto mbalimbali katika kufanikisha ndoto zao za kumiliki ardhi kubwa nchini na kuitumia kujiajiri na kuwaajiri wengine kupitia kilimo.

Akizungumza na vijana hao aliwaambia, “Makundi mengi yameshanitembelea hapa na kueleza changamoto zao lakini GO BIG MOVEMENT mmekuja kitofauti sana na kwa siku nyingi tangu nikiwa waziri mkuu nilikuwa natafuta vijana wa mfano kama ninyi” . Aliongezea kwa kusema, “Mna fursa nyingi sana za kufanya kilimo cha kisasa na hata ufugaji wa kisasa zaidi yangu kwani maarifa yapo nje nje na pia mtaweza kusaidiwa na serikali pamoja na taasisi mbalimbali za kifedha kupitia umoja wenu huu”.
Wajasiriamali wa Go Big Movement wakimsikiliza Mhe. Pinda.

Katika ziara hiyo iliyochukua takribani masaa nane, vijana hao wakiongozwa na kiongozi wao Bw.Meshack Maganga , walipata nafasi ya kumuuliza maswali mbalimbali Mhe.Pinda na kisha kuzunguka katika shamba la ekari hamsini (50) lenye mazao mbalimbali kama vile mapapai, miembe, zabibu, migomba, maparachichi na viazi. Pamoja na kuona kilimo, waliweza pia kuona ufugaji wa nyuki, bata, kuku, ng’ombe, mbuzi , kondoo na hata uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia upepo na kinyesi cha ng’ombe “biogas”.
Mhe. Pinda akiwatembeza vijana wa Go Big shambani kwake.
Baadhi ya vijana wa Go Big Movement wakiwa shambani kwa Mhe. Pinda.
Baadhi ya mifugo iliyopo shambani kwa Mhe.Pinda (Picha na Naamala Samson)

Aidha, waziri mkuu mstaafu alizidi kusisitiza vijana wa kitanzania kujiunga katika vikundi vya kijasiriamali ili waweza kujikwamua kiuchumi. Vilevile katika ziara hiyo, Mhe.Pinda aliweza kuwakutanisha vijana hao na mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw.Nehemia Mchechu ambaye nae hakusita kuwapongeza kwa kuthubutu kuanza safari ya kuwekeza kwenye ardhi hasahasa kufanya kilimo na ufugaji wa kisasa.
Bw. Nehemia Mchechu akisisitiza jambo.
Mizinga ya nyuki shambani kwa Mhe.Pinda.
Bata mzinga shambani kwa Mhe.Pinda.

“Kiukweli ninaliona taifa la Tanzania likiwa linainuka na kufanikiwa kufuta umaskini kupitia kwenu. Na nitajitahidi kuwasaidia kadri niwezavyo ili muweze kutimiza ndoto zenu ikiwa hasa hasa ya kumiliki ardhi na nyumba za bei nafuu kama ilivyo nia ya Shirika la Nyumba la Taifa” Aliongezea Bw.Mchechu.

Baada ya kuzunguka shamba hilo, Mhe. Pinda aliwasisitiza vijana hao kuwa wajasiriamali wabunifu na wenye maono ya kuzalisha vitu vyenye ubora ili viweze kukidhi masoko ya ndani na ya kimataifa kwani tatizo lililopo ni wazalishaji kutofikia viwango vinavyotakiwa na walaji.

Kwa upande wake Bw.Maganga alimshukuru waziri mstaafu huyo kwa kuwapokea kwa heshima kubwa na kuahidi kuendelea kujifunza daima kupitia wakulima, wafugaji na wajasiriamali wengine wakubwa. “Mheshimiwa waziri mkuu mstaafu tukuhakikishie tu haya tuliyojifunza kwako hatutayaacha yapotee, bali tutayafanyia kazi ili kuhakikisha tunajiinua kiuchumi na kuendeleza taifa letu.”
Mhe.Pinda akikabidhiwa fulana na viongozi wa Go Big, kushoto ni Malaika na Bw.Maganga akiwa katikati (Picha na Naamala Samson)
Vijana kutoka umoja wa wajasiriamali wa GO BIG MOVEMENT wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe.Pinda (Picha na Abdilah Lugome).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: