Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe ametangaza rasmi kumruhusu Katibu Mkuu wa chama hicho Dkt. Wilbrod Slaa kuchukua muda wa kupumzika akitafakari uwepo wake ndani ya chama hicho kutokana na yeye kutokubaliana na maamuuzi ya kumpokea waziri mkuu wa zamani ndugu Edward Lowassa.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho wakati wa ufunguzi wa mkutano, Mwenyekiti Freeman Mbowe amesema kuwa chama hicho hakina mgogoro wala ugomvi wowote na katibu mkuu wake kama inavyoelezwa na baadhi ya mitandao bali kinachoendelea ni mchakato wa kidemokrasia wa kukubaliana na kutafakari maamuzi ya kamati kuu.

Wajumbe wakishangilia baada ya mwenyekiti huyo kutangaza maamuzi juu ya katibu mkuu wa chama hicho Dkt. Wilbrod Slaa.

Amesema kuwa mchakato wa kumchukua Edward Lowassa ulipitia katika ngazi zote za vikao ambavyo pia katibu mkuu Dkt. Slaa alikuwepo ila kilichotokea ni kutofautiana kwa mawazo mwishoni mwa mchakato huo jambo ambalo amesema haliwezi kuwarudisha nyuma kwani muda hausubiri na uchaguzi mkuu unakaribia.

Ameongeza kuwa amekuwa na vikao vingi na Dkt. Slaa tangu kutokea kwa mkanganyiko huo vikao ambavyo wamekubaliana kumpa muda kiongozi huyo kutafakari juu ya uwepo wake ndani ya harakati za kuing'oa CCM madarakani wakati chama kinasonga mbele na akishafanya maamuzi ataungana na chama hicho muda na siku yoyote.

Kumekuwa na taarifa zinazotoka katika magazeti kadhaa zinazoeleza kuwa Dkt. Slaa tayari ameshaandika barua ya kuacha kazi na amerudisha vifaa vyote vya chama jambo ambalo mwenyekiti huyo amelipinga na kusema kuwa maneno hayo ni vita inayoendelea baina ya chama hicho dhidi ya wapinzani wake.

Aidha katika hatua iliyokuwa haitarajiwi mwenyekiti huyo aliwahoji wajumbe wote waliokuwa kwenye kikao hicho kama wanakubaliana kumpumzisha Dkt. Slaa kwa muda huku harakati za kujiandaa na uchaguzi zikiendelea ambapo wajumbe wote walisimama na kushangilia ishara ya kukubaliana na maamuzi ya chama hicho ambapo wengi wamekuwa na imani kuwa Dkt. Slaa atarejea na kujiunga tena na chama hicho.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: