Na Mwandishi Wetu, HANDENI

SHIRIKA la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF Tanzania, limejitokeza tena kudhamini Tamasha kubwa la Utamaduni linalojulikana kama ‘Handeni Kwetu’, lililopangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio (Kigoda Stadium), wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Hii ni mara ya pili kwa mfuko huo wa hifadhi kudhamini tamasha hili la utamaduni lilioanza mwaka jana, ambapo lilifanyika kwa mafanikio makubwa kwa kushirikisha vikundi vya ndani na nje ya Handeni, wakiwamo wa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kwamba kujitokeza kwa NSSF ni kitendo cha kiungwana kinacholiweka tukio lao katika kiwango kizuri na mafanikio makubwa.

Alisema kwa kuliangalia hilo, wameamua kutoa haki ya jina, ambapo sasa tamasha lao litakuwa linajulikana kama NSSF Handeni Kwetu, wakiamini kuwa ni ishara nzuri ya ushirikiano baina yao na wadau wote wa shirika hilo.

“Yapo mashirika mengi Tanzania bila kusahau kampuni ambazo zingeweza kudhamini matukio ya aina hii ambayo yana mchango mkubwa kwa taifa letu, lakini baadhi yao yamekuwa magumu mno kudhamini au hata kuyasaidia kwa namna moja ama nyingine.

“Shirika kama NSSF linapoamua kuingia kudhamini ni kuonyesha jinsi wanavyoithamini jamii yao, jambo ambalo kwetu sisi ni furaha kubwa na kuona ipo haja ya kutafuta namna ya kurudisha fadhira kwa wadau hawa muhimu nchini Tanzania,” alisema.

Kwa mujibu wa Mbwana, siku ya tamasha, kutakuwa na shughuli ya kusajili wanachama wapya wa kujiunga na NSSF, ili waweze kunufaika na huduma za mafao kwenye Shirika hilo kubwa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hapa nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: