Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Dkt. Ambwene Mwakyusa (wa kwanza kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano uliofanyika leo ofsini kwao kuhusu tuzo mbalimbali za mashindano ya insha zinazotaraji wa kutolewa kesho katika mkutano wa 22 wa Bodi hiyo (katikati) ni msajili wa Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Bw. Jehad Jehad, (wa kwanza kushoto) ni mtendaji wa bodi hiyo.
Msajili wa bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Jehad Jehada kifafanua jambo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es salaam. (kulia) ni mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, Dkt. Ambwene Mwakyusa.

Na Mwandishi Wetu.

Wanafunzi nchini wamehimizwa kushiriki katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi chini ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi(AQRB) ili kuwajengea uwezo wa udadisi utakaowawezesha kupenda masomo ya Sayansi na kuongeza idadi ya wataalam hao nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Msajili wa bodi hiyo Bw. Jehad Jehad, amesema bodi yao imeimarisha mashindano ya insha kwa wanafunzi wa kidato cha pili ili kuwajengea uwezo na kuondokana na dhana ya ugumu wa masomo ya Sayansi uliopo kwa watu wengi.

“Kwa kuzingatia wanafunzi ni wadau muhimu wanaohitaji kuelewa fani hizi ili hatimae waamue kusoma taaluma hizi, Bodi imeandaa mashindano ya insha kwa wanafunzi wa kidato cha pili, alisema Msajili.

Pia Msajili wa Bodi hiyo alibainisha kuwa endapo wanafunzi wa kidato cha pili watakapofahamu taaluma hizi wataweza kushawishika kusoma masomo ya Sayansi wafikapo kidato cha tatu na hatimae kuamua kusomea taaluma hiyo.

Aidha, Bw. Jehad alifafanua kuwa mwaka jana Bodi ilipokea jumla ya insha 954 kutoka mikoa 13 na kuchambuliwa na jopo la wataalam kwa kutumia vigezo mbalimbali vikiwemo uelewa wa somo linalolengwa, matumizi ya lugha na mantiki katika mtiririko wa mawazo.

Bw. Jehad aliongeza kuwa mashindano ya insha ya mwaka jana yalibeba mada inayozungumzia ‘utaratibu utakaotumika katika mchakato wa kupata majengo mawili ya madarasa na maabara bora kushinda yaliyopo sasa katika shule ikiwa ni pamoja na wataalam wanaotakiwa’.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Ambwene Mwakyusa, amesema kuwa tuzo mbalimbali zinatarajiwa kutolewa kwa washindi hao ikiwemo ya washindi kumi wa kitaifa, Mshindi mmoja kwa kila mkoa ulioshiriki, shule iliyopata mshindi wa kwanza kitaifa pamoja na shule iliyotoa washiriki wengi.

Pia Dkt. Mwakyusa amefafanua kuwa tuzo hizo zinatarajiwa kutolewa kesho katika mkutano wa elimu endelevu wa 22 wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi utakaofanyika katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT).

Jumla ya wanafunzi 109 wamepata tuzo hadi kufikia mwaka 2012 ambapo 66 kati yao ni wasichana tangu tuzo hii kuanzishwa mwaka 2008.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: