Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban ki  Moon akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) siku ya jumanne ambapo alitumia fursa hiyo kuainisha masuala mbalimbali yatakayopewa kipaumbele wakati wa  Mkutano wa 69 wa  Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa  unaoanza wiki ijayo  hapa  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  jijini New York, Marekani.  Mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola ni  moja ya  suala litakalopewa kipaumbele cha pekee wakati wa mkutano huo utakaohudhuriwa na  wa viongozi  zaidi ya 140 wakuu wa nchi na serikali,   viongozi wa  asasi za kiraia, na wakuu wa mashirika mbalimbaliya Kimataifa.
---
Na Mwandishi Maalum, New  New York

 Viongozi  Wakuu wa Nchi na Serikali  zaidi ya 140 kutoka mataifa mbalimbali duniani  wamethibitisha  kuhudhuria na kushiriki  majadiliano ya  jumla wakati wa Mkutano  wa  69 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoanza wiki ijayo.

Akizungumza na  waandishi wa habari hapo siku ya  Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon, amesema,  viongozi hao pamoja na  kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili dunia hivi sasa,  watautumia mkutano huu kujadiliana kwa kina kuhusu  mchango na ushiriki wa jumuiya ya kimataifa katika kuukabili  mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete  ni
miongoni wa viongozi hao 140 na anaongoza 
ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu.

 Akizungumzia zaidi kuhusu mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola na athari zake kwa uhai wa mwanadamu na kwa maendeleo ya  kiuchumi na kijamii,   Ban ki Moon amewaeleza  waandishi hao, kuwa Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuendelea kuufumbia macho na kwamba kadiri inavyochelewa kuutafutia ufumbuzi ndivyo hatari yake inavyozidi kuongezeka.

“Tutatoa kipaumbele cha peke kuhusu ugonjwa wa Ebola ambao umeleta athari kubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika ya Magharibi na maeneo mengine. Siku mbili zijazo (Alhamisi) Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana kwa dharura kuzungumzia mlipuko wa Ebola.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Margaret Chan na Mimi tutazungumza katika mkutano huo” akasema Ban Ki Moon.

Akaongeza kwa kusema wiki ijayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na mkutano wa kilele kuhusu mahitaji ya watu na nchi zilizokabiliwa na ugonjwa wa Ebola. Pamoja na  kujadili na kutafuta mkakati wa pamoja wa kukabiliana na Ebola,  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  anasema viongonzi hao wakuu wa nchi na serikali pia wanatarajiwa  kujadili na kubadilishana  mawazo kuhusu changamoto za mabadiliko ya tabia nchi katika  mkutano utakaofanyika septemba 23.

Mhe. Rais Jakaya  Kikwete ni kati ya  Viongozi walioalikwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  kuhudhuria na kuzungumza katika mkutano huu
muhimu kuhusu  suala zima la mabadiliko ya tabia nchi na  athari zake.

Akielezea zaidi kuhusu mkutano huo wa mabadiliko ya tabianchi, Ban Ki Moon anasema mkutano huo utakuwa na malengo mawili, kwanza ni ukusanya utashi wa kisiasa  ili kufikia makubaliano ya pamoja hapo mwakani katika mkutano utakaofanyika huko Paris , Ufaransa. Na pili kuchukua hatua madhubuti za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu.

Akiainisha zaidi  kuhusu ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa wakati wa Mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa,  Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, amesema,   majadiliano ya Baraza Kuu (General Debate) yatakayoanza septemba 24   yatatumika  kukusanya nguvu za pamoja za  kuushinda umaskini, na kupitisha ajenda za malengo mapya ya maendeleo endelevu .Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya  Mrisho Kikwete atalihutubia Baraza Kuu Septemba 25.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: