Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam. 

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda ambalo linashikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

Kwa nia hiyo, Bulaya anaweza kuwa ametangaza vita dhidi ya Wasira ambaye hivi karibuni akiwa Bunda, alitangaza kukitetea kiti chake hicho katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Julai 8, mwaka huu Wasira akiwa kwenye kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Bunda, alitangaza kuwa atatetea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao, huku akijigamba kuwa yeye ni “mwarobaini wa matatizo” yanayowakabili wakazi wa jimbo hilo.

Kabla ya kutangaza nia hiyo, mara kadhaa Wasira amekuwa akihusishwa na suala la urais na ni mmoja wa makada sita wa CCM ambao walipewa adhabu na chama hicho Februari 18 mwaka huu, baada ya kukutwa na makosa ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Bulaya alisema atagombea ubunge katika Jimbo la Bunda na anamtakia kila heri mpinzani wake huyo (Wasira) katika nafasi ya juu ya urais anayotaka kuwania. Alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuombwa na watu kadhaa kutoka jimboni humo wakiwamo vijana, wazee na kinamama.
“Ninaamini nimepata uzoefu mkubwa katika kipindi hiki cha ubunge wa viti maalumu na ninawataka wabunge wenzangu wa viti maalumu waone kuwa nafasi hiyo ni fursa ya kujifunza, lakini mwisho wa yote lazima urudi jimboni,” alisema.

“Hii ni mara ya kwanza nasema hapa. Nitagombea ubunge Jimbo la Bunda kwa kuwa nimeombwa sana na vijana, wazee na ni mara nyingi nimekuwa nikisema bado muda, lakini sasa umebaki muda mfupi hivyo niseme tu kwamba nitagombea. Uongozi ni mbio za kupokezana vijiti. Wasira ni kama baba yangu na sina ugomvi naye na namtakia kila la heri katika position (nafasi) yake nyingine anayoitaka,” alisema.

Kuhusu madai kwamba Wasira anafikiria kuwania urais, alisema, “Naona ni uamuzi sahihi amefanya, kwani amekuwa mbunge tangu mimi nazaliwa mwaka 1980 ameona kwamba ni kweli hii position (nafasi) ya chini ameshaitumikia sana, hivyo ameona katika uzoefu alionao labda ajaribu katika nafasi ya urais.”

Bulaya alisema si kwamba ameamua kugombea ubunge wa Bunda kwa kuwa Wasira anataka urais, bali viti maalumu alipo hivi sasa ni njia ya kupata uzoefu na kujifunza katika kuelekea kugombea ubunge wa jimbo.

“Ili kuondoa suala la kwamba viti maalumu ni vya kupewa siyo kwamba nasema vifutwe, lakini unaweza ukawekwa utaratibu mwingine wa kumpa mwanamke uzoefu katika ngazi ya kibunge,” alisema na kuongeza;

“Lakini unapopewa hebu itendee haki hiyo fursa, kama mtu umeingia viti maalumu unajifunza na unakwenda kugombea na huko kuna kushinda na kushindwa lakini ni lazima nionyeshe hii fursa nimepewa naweza kwenda kushindana na wanaume.”

Alisema hilo ni jambo la msingi kwa kuwa huwezi kulemaa kwa kuwa mbunge wa viti maalumu bila kujifunza na kukaa miaka hadi 15 kwenye ubunge wa aina hiyohiyo kwani wako wengine wanaotakiwa kupata nafasi hiyo ili wajifunze na kwenda majimboni. 

HABARI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: