Mwanamuziki wa nyimbo za Injili nchini, Rose MuhandoMWANAMUZIKI wa nyimbo za Injili nchini, Rose Muhando anasakwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar baada ya mchungaji mmoja wa Kinigeria anayefanya shughuli zake nchini DR Congo,  Kabagambe Tchanda kumshitaki akidai kumlipa fedha ili akafanye onesho badala yake akaingia mitini.

Uchunguzi uliofanywa na Uwazi ndani ya jeshi hilo, umegundua kuwa kuna madai hayo na kwamba mchungaji huyo alitua jijini Dar na kufanya mazungumzo na Rose kwa ajili ya kwenda kutumbuiza nchini DR Congo, Julai mwaka huu katika mkutano uliohusisha wageni kutoka Ulaya na kukubaliana amlipe Dola za Marekani 5,000 (zaidi ya shilingi milioni 8).

Kwa mujibu wa chanzo, ilidaiwa kuwa mchungaji huyo alimkabidhi Rose dola 1,900 kama utangulizi na kubaki dola 3,100 ambazo angemlipa baada ya onesho. Makabidhiano hayo yalifanyika Magomeni ya Mwembechai jijini Dar.

Kutokana na sekeseke hilo, mwandishi wetu alimsaka mchungaji huyo na alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa madai hayo, alikiri na kusema alimuamini sana Rose lakini cha ajabu mambo yamekuwa tofauti kwa kuwa hakufika kwenye tamasha.

Mchungaji huyo aliendelea kudai kuwa, kinachomuuma zaidi ni kwamba, Rose hataki kumrudishia fedha zake na badala yake amekuwa akimzungusha na chenga kibao.

“Siamini kabisa kama Rose angeweza kufanya vile maana yeye ni mtumishi wa Mungu, sasa kwa nini afanye mambo yasiyompendeza Bwana? Nashangaa sana, sijui hata ni nini kimemuharibu huyu! Nikimpigia simu akipokea kesho haziishi.

“Anashindwa kuwa na utu maana mimi nimeishiwa fedha naishi kwa shida hapa nchini, angenipatia hizo pesa zingenisaidia sana maana ujio wangu huu ni kwa sababu ya kudai hizo pesa tu, ndiyo maana nikaamua kulifikisha suala hili kwenye vyombo vya dola baada ya kuona hatuelewani,” alisema.

Ili kuweka sawa mzani wa habari, paparazi wetu alimtafuta Rose Muhando kupitia simu yake ya mkononi ambayo iliita bila ya kupokelewa licha ya kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi aliamua kukaa kimya mpaka gazeti linakwenda mtamboni.

Kesi imefunguliwa katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ kwa jalada namba KJN/RB/7122/14 KUJIPATIA PESA KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: