Mheshimiwa Angellah Kairuki(MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria akisalimiana na askari Magereza wa Gereza la Segerea mara alipofanya ziara katika Gereza hilo kwa lengo la kuzungumza na mahabusu na wafungwa na kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuzitatua. Nyuma ya Mheshimiwa Kairuki ni Bw. Malewo, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Jeshi la Magereza.
Kamishna Malewo akifafanua jambo wakati akiwatambulisha maafisa wa Jeshi la Magereza ambao wameambatana naye katika ziara ya Mhe. Naibu Waziri ya kulitembelea Gereza la Segereza la Segerea.
Mheshimiwa Kairuki akizungumza jambo na watumishi wa jeshi la polisi na magereza (hawapo pichani) katika ziara yake Gereza la Ukonga. Katika picha kushoto kwa Mhe. Kairuki ni Mhe. Pereira Silima, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Ayub Mwenda, Mkurugenzi Msaidizi – Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali – Divisheni ya Mashtaka na Bw. Mwaisabila ACP, Mkuu wa Gereza la Ukonga. Kulia kwa Naibu Waziri ni Bw. Malewo, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji Jeshi la Magereza, Maafisa wengine ni Bw. Bukuku, Mkuu wa Magereza Mkoa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Upelelezi.
Mhe. Kairuki na msafafara wake wakisalimiana na maafisa wa Jeshi la Magereza wa Ukonga waliofika kumpokea alipotembelea gereza hilo katika mwendelezo wa ziara yake wa kuzungumza na wafungwa na mahabusu, kusikiliza kero zao na kuangalia namna ya kuzitafutia ufumbuzi
---
Katika mwendelezo wa uboreshaji wa Sekta ya Sheria Nchini, hivi karibuni Mhe. Angellah Kairuki(MB), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria amefanya ziara katika Magereza ya Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Lengo la ziara hiyo, pamoja na mambo mengine, ni kusikiliza kero za wafungwa na mahabusu na kuangalia namna ya kuzitatua. Hii ni pamoja na kuangalia namna ya kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa katika magereza yote ya Tanzania.

Magereza yaliyotembelewa na Mheshimiwa Kairuki katika ziara yake ni pamoja na Segerea na Ukonga kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Kigongoni lililoko Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Katika ziara hiyo Mhe. Kairuki aliambatana na Maafisa Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Jeshi la Magereza na Maafisa wa Jeshi la Polisi-Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi), Mahakama ya Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali – Divisheni ya Mashtaka.

Kero kubwa zinazolalamikiwa na mahabusu ambazo walimweleza Mhe. Kairuki kwa upande mmoja ni pamoja na kubambikizwa kesi, upelelezi wa mashauri yao kuchukua muda mrefu hususan kwa kesi za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, masharti magumu ya dhamana ambayo wamekuwa wakipewa na Mahakama na kusababisha wao kukaa rumande kwa kushindwa kuyatimiza na hivyo kusababisha msongamano katika magereza hayo na kutokupangiwa vikao na Mahakama Kuu kusikiliza kesi zao baada ya upelelezi kukamilika. Kwa upande wa pili wafungwa walikuwa na kilio cha kucheleweshewa nakala za hukumu, vitabu vya rufaa na mienendo ya kesi ili kuwawezesha kukata rufaa.

Mheshimiwa Kairuki aliahidi kwamba Wizara yake kwa kushirikiana na Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Jeshi Polisi kwa pamoja watazifuatilia kero hizo na kutatua kero ya kutokupatikana kwa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri kwa wakati, kuchelewa kwa vitabu vya rufaa, uhaba wa vikao vya Mahakama Kuu na ucheleweshwaji wa upelelezi.

Zaidi ya hayo, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwasihi wale wanaopata fursa ya kutoka magerezani kwa kupata msamaha wa Mheshimiwa Rais kuendelea kuwa raia wema katika jamii. Vilevile, Mheshimiwa Kairuki aliwahakikishia wafungwa na mahabusu kwamba Serikali kupitia Jukwaa la Haki Jinai itaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha kwamba msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani unatatuliwa, usikilizwaji wa kesi unakuwa na ufanisi na kuangalia namna ya kuondoa ubambikizwaji wa kesi. Kwa upande mwingine aliwaasa Jeshi la Polisi na Magereza kuzingatia masuala ya haki za binadamu wanapotekeleza majukumu yao katika kuwahudumia mahabusu na wafungwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: