Na Veronica Kazimoto – MAELEZO, Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekanusha taarifa ya kuachiwa huru kwa mtuhumiwa wa ujangili Bw. Frank William Silangei maarufu kwa jina la “Ojung’s Mwarusha” mkazi wa Ngaramtoni Kibaoni iliyotolewa na gazeti moja la kila wiki.

Akizungumza katika mahojiano kwa njia ya simu na Idara ya habari MAELEZO leo jijini Dar es Salaam, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alisema kuwa mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 32 hivi sasa yuko mahabusu na taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea kufanyika.

Kamanda Sabas alieleza kuwa mtuhumiwa Silangei hajaachiwa huru kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo linalotoka kila Alhamis katika ukurasa wake wa kwanza na wa pili na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo liko makini katika kutekeleza majukumu yake.

“Si kweli hajaachiwa, natamani ungekuwa hapa Arusha nikakupeleka mahabusu ukamuona mtuhumiwa kwa macho yako”, amesema Kamanda Sabas.

Kamanda Liberatus Sabas alisema Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya ujangili vinatokomezwa na yeyote atakayehusika na vitendo hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: