(Wakuu wa wilaya wapya wa mkoa wa Kagera wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kagera mara baada ya kula kiapo mwaka jana 2012).
---
Mkoa wa Kagera unapatikana kaskazini magharibi mwa nchi ya Tanzania. Makao makuu ya mkoa yapo katika mji wa Bukoba umbali wa kilometa 1500 kutoka Dar es Salaam, mkoa huu unapakana na nchi ya Uganda kwa kaskazini, Rwanda na Burundi kwa upande wa magharibi mkoa wa Kigoma, Mwanza kwa upande wa kusini na ziwa Victoria kwa upande wa mashariki. Vile vile mkoa wa Kagera uko kusini mwa ikweta kati ya 1 “00” na 2”45” latitudi. Kwa Iongitudo uko katika nyuzi 30”25” na 32”40” Mashariki mwa ‘greenwich'.
Mkoa wa Kagera ulijulikana kama “Ziwa Magharibi” jina hili lilidumu katika kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru mpaka mwaka 1979 baada ya vita kati ya Tanzania na Uganda.
Mkoa ulipata jina hili kutokana na mto Kagera ambao hutiririsha maji yake kutoka Rwanda kupitia kaskazini na kumwaga maji yake katika ziwa Victoria.
Mkoa wa Kagera una jumla ya eneo la kilomita za mraba 39,168 kati ya hizo kilometa za mraba 28,513 ni eneo la nchi kavu za kilomita 10,655 ni eneo la maji. Ukiacha mbali wilaya za Biharamulo na Chato ambazo ni tambarare sehemu kubwa ya mkoa ni yenye milima na vilima vilivyogawanywa na mabonde yenye matingatinga. Upande wa magharibi wa mkoa mito mingi inamwaga maji yale katika mto Kagera ambao nao humwaga maji yake katika ziwa Victoria.
Hali ya hewa
Hali ya hewa ya mkoa wa Kagera kwa ujumla ni ya joto la wastani wa 26.02 sentigredi. Mvua zinanyesha kwa wastani wa milimita 800-1,100 kwa mwaka kati ya mwezi Septemba na Januari na kati ya mwezi Machi na Mei. Mvua hizi ndizo zinazowezesha kuwepo kwauoto wa asili wa kuvutia katika maeneo mengi ya mkoa. Kwa miaka ya kawaida mkoa hupata mvua za uhakika za vuli na masika ambazo ni muhium kwa shughuli za kilimo na ufugaji.
UTAWALA
Wakati tunapata UHURU, mkoa wa Kagera ulikuwa na jumla ya wilaya nne (4), wilaya hizo ni Ngara ambayo ilianzishwa mwaka 1947, Biharamulo, Bukoba, na Karagwe mwaka 1958 ambayo ilizinduliwa rasmi na gavana wa kiingereza Sir Richard Turnbul. Aidha, mwaka 1975 wilaya mpya ya Muleba ilianzishwa kutoka kwenye wilaya ya Bukoba na mwaka 2007 wilaya ya Chato na Missenyi zilianzishwa na kuunda jumla ya wilaya 7 za mkoa wa Kagera.
Kwa sasa mkoa wa Kagera una jumla ya wilaya saba (7) na halmashauri 8. Wilaya hizo ni Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe, Missenyi na Ngara. Halmashauri ni Bukoba Manispaa, halmashauri ya wilaya ya Bukoba, Muleba, Biharamulo, Ngara, Chato, Karagwe na Missenyi.
Kisiasa mkoa una jumla ya majimbo 10 ya uchaguzi (Muleba 2, Karagwe 2, Ngara 1, Biharamulo 1, Missenyi 1, Bukoba Manispaa 1, Bukoba Vijijini 1 na Chato jimbo 1).
IDADI YA WATU
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 1967 mkoa ulikuwa na watu 658,712, mwaka 1978 watu 1,009,379, mwaka 1988 mkoa ulikuwa na watu 1,326,183 na mwaka 2002 watu 2,033,888. Ongezeko la idadi ya watu lilikuwa kwa wastani wa asilimia 2.7. Aidha, mwaka 2011 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002 mkoa unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,746,058.
Halmashauri Ya Wilaya
|
Idadi ya Watu
| ||||
1978
|
1988
|
2002
| MATOKEO YA 2011 | ||
Missenyi |
-
|
-
|
-
|
174,889
| |
Bukoba (V)
|
296,462
|
343,950
|
395,130
|
467,129
| |
Bukoba (M)
|
36,914
|
47,009
|
81,221
|
153,016
| |
Muleba
|
217,493
|
274,447
|
386,328
|
492,404
| |
Chato |
-
|
-
|
-
|
383,162
| |
Biharamulo
|
165,580
|
209,524
|
410,794
|
252,218
| |
Karagwe
|
185,013
|
292,589
|
425,476
|
542,517
| |
Ngara
|
107,917
|
158,658
|
334,939
|
422,044
| |
JUMLA
|
1,000,379
|
1,326,183
|
2,033,888
|
2,746,058
|
Chanzo: Ofisi Kuu ya Takwimu Taifa (NBS) , 2011
HISTORIA YA MKOA WA KAGERA
Mkoa huu haukuitwa Kagera bali ulikuwa moja ya maeneo yaliounda jimbo lililoitwa Lake Province. Jimbo hili lilijumuisha Wilaya ya Bukoba, Musoma, Shinyanga na Tabora. Baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa ‘West Lake Region' (Ziwa Magharibi) na kujumuisha Wilaya 4 za Ngara, Biharamuro, Karagwe na Bukoba.
Kabla na baada ya kuja kwa wakoloni mkoa wa Kagera ulikuwa na utawala wa Kimila (Chiefdoms) uliogawanyika katika himaya 8. Himaya hizo ni pamoja na Kyamutwara, Kihanja (Kanazi), Kiziba, Ihangiro, Bugabo, Karagwe, Biharamulo (Rusubi) na Maruku (Bukara).
Baadhi ya Watemi waliotawala himaya hizo ni pamoja na Emmanuel Rukamba (Kyamtwara), Rumanyika (Karagwe), Kasusura (Biharamulo), Lugomola (Bukara), Rutinwa (Kiziba), Kayoza (Bugabo), Kahigi (Kihanja) na Nyarubamba (Ihangiro). Kila mtemi alikuwa na walinzi wake walioitwa Warugaruga.
Wakazi wa asili ya Kagera ni wabantu na wengi wao wana asili ya Bunyoro. Wanaongea lugha sawa na ile ya Wanyoro, Wanyankole, Watoro na Wakiga. Busubi na Bugufi wana lugha na desturi sawa na Watusi, Wahutu na Waha. Lakini makabila hayo ni ya Wabantu wa Ziwa (Interlacustrine Bantu) na yanafanana mila na desturi. Makundi hayo yaligawanyika kati ya wachungaji (Bahima) ambao walitawala na wakulima (Bairu) ambao walitawaliwa na mara nyingi kudharauliwa. Bahima (Balangira) walikuwa na koo chache zipatazo 20 na walitawaliwa na Wahinda, Wabito na Wankango.
Bairu walikuwa na Koo kama 130 zenye mashina 24 ambayo kiasili walikuwa Bairu lakini kwa kuoa katika Bahima au kufanya kazi kwa Watemi walipandishwa hadhi na kuwa Bahima (Batware). Kila ukoo uliitwa jina la Baba mwanzilishi wake na kina ukoo ulikuwa na kitu walichokatazwa kula (Omuziro) na mnyama walioshirikishwa nae (Ekyerumono).
Mkoa ulibadilishwa jina na kuitwa Kagera mwaka 1979 baada ya vita ya Tanzania na Uganda. Chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo wakati huo Capt. Peter Kafanabo jina la Kagera lilipendekezwa kwa sababu ya mto Kagera unaogusa sehemu kubwa ya Wilaya zote zinazounda Mkoa wa Kagera.
Uchumi wa wenyeji wa Kagera ulijikita katika mashamba ya migomba. Chakula chao kikuu ni ndizi katika aina zake mbalimbali. Katika mashamba yao hulima mazao mengine kufuatana na msimu. Mazao hayo ni pamoja na maharage, mihogo, mahindi na mboga. Baada ya kuja kwa wazungu waliongeza ulimaji wa kahawa kama zao la biashara lililowasaidia kujiongea kipato.
TUTAENDELEA KESHO... UTAJIFUNZA VITU VINGI ZAIDI...
Toa Maoni Yako:
0 comments: