WATANZANIA na mashabiki wa sanaa hapa
nchini bado wapo kwenye majonzi ya kufiwa na msanii wao, Sadiki Juma
Kilowoko, maarufu kama Sajuki, aliyekufa Januari 2, katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili na kuzikwa Junuari nne katika makaburi ya Kisutu.
Kutokana na msiba wake kugonga vichwa
vya watu wengi, mazishi yake yalihudhuliwa na viongozi mbalimbali wa
Kitaifa, wakiwamo wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Jakaya Mrisho Kikwete.
Yalikuwa ni majonzi tupu. Kila mmoja
alikuwa na hisia kwanini Sajuki amekufa, huku kumbukumbu ya ugonjwa
wake na kusababisha kuchangiwa zikiendelea kuranda randa katika
vichwa vyao, hasa wakiangalia picha za mazishi yake.
Pamoja na hayo, lakini kwa bahati
mbaya, wapo watu ambao kwa namna moja ama nyingine waliutumia msiba
huo kama sehemu ya kuuza sura. Nikiambiwa niwataje watu hao, hakika
siwezi kushindwa kuwataja wasanii wa filamu.
Wengi waliutumia kama fasheni tu. Haya
yametokana na baadhi yao kuangaliwa nyuso zao, hisia zao pamoja na
bashasha kubwa walizokuwa nazo. Kingine kilitokana na lugha zao,
wakati wanawasiliana na mmoja hadi mmoja.
Kwakweli umependeza sana shosti chombo
cha wapi hicho? Hii ni kauli ya msanii mmoja aliyenaswa naa kipaza
sauti chetu akimuuliza mwenzake alipomuona amevaa nguo ambazo kwa
mujibu wa wasanii hao, ilikuwa nzuri.
Kauli kama hizi ndo chachu ya wasanii
hao. Hii imetokana na kupenda kutumia vifo vya wenzao kuuza sura zao.
Wanajua kuwa kwenye msiba ni mahali kwa kuonana hata na wale ambao
wamekuwa adimu kuonekana mitaani.
Pia wanajua kuwa ni mahali kwa
kuonekana na watu wa kipato cha chini, kipato cha juu na jamii yote
ambayo kwa bahati nzuri, kunapotokea tatizo la msiba huguswa. Haya
yalitokea pia katika msiba wa Hussein Mkiety maarufu kama
Shaaromillionea.
Baadhi ya wasanii walikwenda na nguo
fupi mno maarufu kama (vimini) katika msiba ambao eneo kama Lusanga,
wilayani Muheza mkoani Tanga inajulikana mazingira yake.
Pia yalitokea katika msiba wa marehemu
Steven Kanumba ambapo wasanii hasa wasichana waliutumia sana
kuonyesha urembo wao.
Tukirudi katika msiba wa Sajuki ambaye
bado yupo kichwani mwa Watanzania kutokana na msiba wake kuwa mbichi,
tulishuhudia baadhi yao wakigongana vichwa kumkimbilia rais kwa ajili
ya kumpa mkono na mengineyo.
Hata hivyo haitoshi, wengine walikuwa
na mawazo tofauti na misiba, wakikutwa wakipiga soga pembeni mwa
nyumba yenye msiba, huku mazungumzo yao wakiyajua yenyewe. Kwakweli
si jambo laa busara.
Wasanii na jamii ibadilike. Kutumia
msiba wa mtu kuonyesha umaarufu wako ni kitendo cha kifedhuli mno na
hakiwezi kuchekewa na watu wenye mioyo ya huruma. Kunapotokea msiba,
kila mmoja awe na uchungu wa kweli.
Lakini kwenda msibani kuuza sura, jina
kuna siku tutashuhudia watu wakipopolewa kwa mawe na wenye uchungu wa
kweli na ndugu zao. Kwa kusema haya machache niliyoyaona katika msiba
wa Sajuki, nashawishika kusema kwenye msiba, wengineo huenda kufanya
biashara zao na vinguo vya ajabu, mafuta ya ajabu ili waonakane
warembo, hasa wanawake.
Toa Maoni Yako:
0 comments: