Na Veronica Kazimoto – MAELEZO, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo (pichani) ametangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa
Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili mwaka 2012, ambapo kiwango cha
ufaulu kimepanda kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia
64.55 mwaka 2012.
Matokeo hayo yametangazwa mbele
ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ambapo idadi ya
watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 430,327, kati yao
wasichana walikuwa 205,476 na wavulana 224,851, ikiwa ni upungufu wa
watahiniwa 36,240 ikilinganishwa na mwaka 2011 ambao walikuwa 466,567.
“Watahiniwa 386,271 sawa na
asilimia 89.76 ya waliosajiliwa, walifanya mtihani wakiwemo wasichana
187,244 na wavulana 199,027, watahiniwa 44,056 sawa na asilimia 10.24
hawakufanya mtihani, kati yao wasichana ni 18,231 na wavulana 25,825”
amesema Mulugo.
Aidha Waziri Mulugo amefafanua
kuwa watahiniwa 136,946 ambao wameshindwa kupata wastani wa ufaulu wa
alama 30 na wale waliofutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu
watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka 2013.
“Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri
kidato si adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa mwanafunzi kuweza
kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari, hivyo ni matumaini
yangu kuwa wanafunzi hawa watafanya bidii katika kujifunza na
kuzingatia masomo ili waweze kufaulu masomo yao katika kiwango
kinachotakiwa” amesisitiza Mulugo.
Mtihani wa Taifa wa Elimu ya
Sekondari Kidato cha Pili ulifanyika nchini kote kuanzia tarehe 05
Novemba, 2012 na kumalizika tarehe 16 Novemba, 2012 kukiwa na jumla ya
vituo 4,304 vilivyosajili watahiniwa, sawa na ongezeko la vituo 117
ikilinganishwa na ile ya mwaka 2011.
Toa Maoni Yako:
0 comments: