Shindano la kumsaka malkia wa shindano la Miss East Africa 2012 linalofanyika kwa mara ya tano sasa litarindima Desemba 21 Ijumaa hii kwenye ukumbi wenye hadhi na wa kisasa wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mratibu wa shindano hili, Rena Callist, kila kitu kiko tayari hivyo mashabiki wa masuala ya urembo wajitokeze kwa wingi siku hiyo kuja kumuona mrembo wa n hi gani atatoka akinema kwa madaha baada ya kuibuka na ushindi.
Taji la Miss East Africa linaloshikiliwa na mrembo kutoka Rwanda, Cyntia Akazuba, ndiye atakayemvika taji mshindi atakayetwaa taji hilo Ijumaa.
Akizungumzia kuhusu maandalizi ya warembo hao kutoka nchi mbalimbali, Rena anasema wamefurahia mazingira ya nchi na kambi kwa ujumla.
“Warembo hawa wamepata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hivyo tunatarajia watakuwa mabalozi wetu wazuri baada ya shindano,” anasema Callist.
“Zawadi zenye thamani ya sh mil.100 zitatolewa kwa washindi wa mwaka huu huku kila mmoja akitarajiwa kuondoka akiwa mwenye tabasamu pana,” anasema Callist.
Mshindi wa kwanza atapata jumla ya dola za Kimarekani 30,000 pamoja na gari aina ya Mazda lenye thamani ya dola 15,000 na mkataba wa kufanya kazi na Oganaizesheni ya Miss East Africa wenye thamani ya dola 15,000.
Mshindi wa pili atapata zawadi zenye thamani ya dola 8,000 ikiwa ni pamoja na kitita cha dola 2,000 na mkataba wa kufanya kazi na Oganaizesheni ya Miss East Africa wenye thamani ya dola 6,000.
Mshindi wa tatu atapata zawadi zenye thamani ya dola 5,000 pamoja na fedha taslimu dola 1,500 na mkataba wa kufanya na Oganazesheni ya Miss East Africa wenye thamani ya dola 3,500.
Shindano hili la kimataifa linashirikisha warembo kutoka nchi za Tanzania (mwenyeji), Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Djibouti, Eritrea, Sudan, Ethiopia, Malawi, Seychelles na South Sudan; na warembo mbalimbali wa Afrika Mashariki walioshindana katika nchi mbalimbali za Ulaya ambazo ni Ubelgiji, Ufaransa na Uholanzi.
Mashindano ya Miss East Africa yanaandaliwa na kumilikiwa na Kampuni ya Rena Events Ltd ya jijini Dar es Salaam.
Callist anawataja wadhamini wa shindano hilo kuwa ni Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, TANAPA, Shirika la Ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines), DTP, Ako Catering, Darlings Hair, Seascape Hotel, Satguru na Clouds FM.
Baadhi ya majina ya warembo ni Umwari Neema ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha Kigali Institute of Education (KIE) na pia ni mfanyakazi wa kampuni ya simu za mkononi ya Tigo jijini Kigali.
Mrembo atakayeiwakilisha Kenya ni Joan Wambui Ndicho (18) mwenye urefu wa futi 5.8 na anayetarajia kujiunga na Chuo Kikuu Kishiriki cha Machakos kusomea mambo ya utalii.
Mrembo wa Djibout ni Assia Mohamed (22) na Sarah Nyamwenge kutoka nchini Uganda.
Shindano hili litashuhudiwa na mamilioni ya watu duniani kupitia kwenye runinga zao na pia kwa njia ya mtandao ambapo yatautangaza utalii wa nchi yetu ipasavyo kwa kiasi kikubwa na pia kujenga umoja wa Afrika Mashariki na kudumisha utamaduni wa ukanda huu wa Afrika.
Mashindano ya Miss East Africa yaliasisiwa mwaka 1996 na yalifanyika jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments: