Mwenyekiti wa Chama cha Democrasia na Maendeleo- CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe alikiongea na wanahabari leo.

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyoketi kikao chake cha kawaida kwa siku mbili, Desemba 15-16, 2012, katika Hotel ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam, imemaliza kikao chake Desemba 16, usiku.

Pamoja na kwamba maazimio yote ya kikao hicho yatatolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari, Desemba 18, 2012, huu ni ufafanuzi wa awali kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazowakanganya wanachama na Watanzania kwa ujumla, zilizoandikwa tangu jana Jumapili na Jumatatu, katika baadhi ya vyombo vya habari.

Wanahabari wakifuatilia mkutano wakati Mwenyekiti wa Chama cha Democrasia na Maendeleo- CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe akiongea na wanahabari leo.

Mbali ya kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo kupokea taarifa ya hatua kadhaa za utekelezaji wa maazimio yatokanayo na vikao viwili vilivyotangulia, Kamati Kuu pia ilijadili hali ya siasa nchini, mchakato wa Katiba Mpya na Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).

Kamati Kuu pia ilipokea taarifa ya mwenendo wa chama kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambapo ilijadili pia kasoro za utendaji wa viongozi wa chama katika Wilaya ya Karatu.

Kamati Kuu ilichukua uamuzi wa kusimamisha uongozi mzima wa Wilaya ya Karatu na kuweka shughuli za utendaji wa chama chini ya uangalizi wa Kamati Kuu mpaka hapo itakapotolewa maagizo mengine baadae.

Aidha, Kamati Kuu pia ilipokea na kujadili mwenendo wa utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa taasisi za kiserikali wanaotokana na CHADEMA, hasa katika masuala ya ardhi na maji Wilayani Karatu.

Kikao pia kilibaini kuwa taarifa zinazohusu masuala hayo ya maji na ardhi ni tofauti na namna zilivyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari. Aidha kutokana na mjadala, iliazimiwa hatua kadhaa zichukuliwe, ambazo umma utaarifiwa katika tamko la Kamati Kuu litakalotolewa kupitia waandishi wa habari.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: