Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali na kumpa pole Katibu wa
Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soraga ambaye amelazwa katika chumba
cha dharura katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia majeraha ya
usoni na kifuani yaliyotokana na kurushiwa Tindikali na watu
wasiojulikana wakati akifanya mazoezi katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe
mjini Unguja juzi.
---
Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la
Polisi Zanzibar, limeanza uchunguzi na msako wa kuwatafuta wale wote
waliohusika kwenye tukio la kumwagia maji makali Katibu wa Mufti wa
Zanzibar Sheikhe Fadhil Soraga, alfajiri ya leo (Novemba 6, 2012) wakati
akiwa mazoezini mjini Zanzibar.
Taarifa
ya Afisa Habari Mkuu wa Jeshi hilo Visiwani Zanzibar Inspekta Mohammed
Mhina, imesema kuwa Jeshi la Polisi Visiwani humo limeanza uchunguzi
na msako mkali wa kuwabaini na kuwatia mabaroni wale wote waliohusika
katika shambulio la Katibu huyo wa Mufti Zanzibar.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari kwa nyakati tofauti leo, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar ACP Yusufu Ilembo na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, ACP
Aziz Juma Mohammed, wamesema kuwa Waandishi wa Habari Ofisini kwake,
Kamanda Ilembo amesema Jeshi la Polisi limesikitishwa na kitendo
alichofanyiwa Sheikhe Soraga na kwamba wanakichukulia kama kitendo cha
kihalifu.
Kamanda
Ilembo amesema Jeshi la Polisi litahakikisha kuwa wale wote waliohusika
na tukio hilo, wanabainika, kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu
tuhuma zinazowakabili na hatimaye sheria kuchukua mkondo wake.
Kwa
upande wake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP
Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa tayari ameunda kikosi kazi cha
Makachero watakaokusanya taarifa za kubaini njama na watekelezaji wa
tukio hilo la kumwagia sheikhe huyo maji hayo yenye ukali.
Amesema Shekhe Soraga, alimwagiwa maji hayo katika viwanja vya
Mabata vilivyopo karibu na Msikiti wa Msumbiji akitokea upande wa
Uwanja wa Michezo wa Aman kwenda Mwanakwerekwe ambapo akiwa katika eneo
hilo alikutana na mtu mmoja ambaye naye alionekana kama mchukua mazoezi
akitokea upande wa Mwanakwerekwe kuelekea Uwanja wa Aman na walipokuwa
wakipishana ndipo alipomwagiwa machoni maji hayo yenye ukali.
Amesema
baada ya tukio hilo Sheikhe Soraga alikaa chini kwa maumivu na baada ya
kuda kidogo alipata wasamalia wema na kumchukua hadi kwenye Hospitali
Kuu ya Mnazi Mmoja ambako alipatiwa matibabu ya awali kabla ya
kusafirishwa kwa ndege ya Serikali kwenda Dar es Salaam ambako amelazwa
katika Hospitali ya Agha Khan kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Naye Mufti wa Zanzibar Sheikhe Salehe Kabi, amewataka Wananchi wa Zanzibar kuacha visa vya kulipiziana visasi vitendo ambavyo vinaweza kuleta vurugu na kuzua mtafaruku katika nchi yetu.
Aidha
amewataka watu wote kuwa wamoja na kushirikiana kwa kila jambo na
kwamba tofauti za rangi, kabila, dini na itikadi za kisiasa ziwe chanzo
cha mafarakano ya Umoja wetu.
Kwenye
uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar, Sheikhe Soranga,
alisindikizwa na Makamu wa Pili wa Rais balozi Seif Ali Iddi, Mkuu wa
Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mh. Abdallah Mwinyi na viongozi wengine
wa vyombo vya ulinzi na usalama na Mashekhe.
Wakati
Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kujua aina ya maji hayo
pamoja na kuwapata waliohusika katika tukio hilo, Jeshi hilo limewataka
wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano wa kuwabaini wale wote
waliohusika katika tukio hilo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: