Na Mohammed Mhina, Zanzibar 

Zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa wilaya ya Kusini Unguja Zanzibar wamejitokeza kujiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa wengi wao wakiwa ni vijana.

Mkurugenzi wa Vitambulivyo vya Taifa Zanzibar Bw. Vuai Mussa Suleiman, amesema kuwa zoezi hilo lililoanza mwanzoni mwa mwezi huu  limeonyesha mafanikio na Jumatatu ijayo ya Oktoba 29, 2012 zoezi hilo litaingia katika wilaya ya Kati katika mkoa huo wa Kusini Unguja.

Bw. Vuai alikuwa akitoa taarifa kwa Waandishi wa Habari aliofuatananao katika ziara ya pamoja ya kuvitembelea vituo hivyo vya kujiandikishia katika wilaya ya Kusini unguja zoezi ambalo lilianza Oktoba 15, mwaka huu na linatarajiwa kumalizika kesho Alhamisi Oktoba 26, 2012.

Bw. Vuai amewataka wananchi wa wilaya zingine kujiandaa kwa kupiga kopi baadhi ya vielelezo muhimu vikiwemo vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo.

Wakati wa ziara hiyo baadhi ya wasimamizi na masheha waliopo katika vituo hivyo wameelezea mafanikio na changamoto zinazojitokeza ambapo wamesema baadhi ya watu wanaofika kujiandikisha hawaelewi hata maana na foto kopi.

Msimamizi wa Kituo cha Bwejuu Bw. Khamisi Mabrouk Mbaraka,baadhi ya watu wanaofika katika vituo vyao wanapeleka hati halisi pasipo na kopi. 

Nao baadhi ya Mashehe wamesema kuwa hakuna uwezekano wa mtu asiyehusika kujipenyeza na kujiandikisha kwa sababu watu wote wakiwemo wasio na vitambulisho vya Uzanzibar Mkazi wanaoshi katika shehia zao wameorodheshwa majina na kwamba ikijitokeza utata Sheha anawajibika kulitatua kwa kupitia kumbukumbu za wakazi wa eneo lake.

Akizungumza katika kituo cha Bwejuu, mmoja ya watu waliofika kujiandikisha Bi. Mwakito Mkadamu, ameelezea umuhimu wa vitambulisho hivyo kwa jinsi alivyoelimishwa kupitia vyombo vya habari na kusema kuwa kinaweza kumsaidia katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kifamilia na kiuchumi.

Miongoni mwa watui wanaojiandikisha kupata vitambulisho hivyo wapo wa kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania bara wanaoishi Zanzibar kwa shughuli binafsi na za kikazi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: