Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la KISITULI S/O MWALISHE, Mgogo mwenye umri wa miaka (53) na mkulima wa Bahi ameuwawa kwa kuchomwa na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumzia Tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw. Zelothe Stephen (pichani), Alisema Tukio hilo limetokea siku ya Jumanne tarehe 10/07/2012 majira ya saa sita usiku katika kijiji cha Bahi Sokoni, Kitongoji cha Mugu kata ya Bahi na wilaya ya Bahi.
Alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo aliyejulikana kwa jina la JEROME S/O MAZENGO, Mgogo na mwenye umri wa miaka (45) amekamatwa na anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya Upelelezi zaidi.
“Marehemu alikuwa amealikwa nyumbani kwa rafiki yake huyo bwana JEROME S/O MAZENGO na wakaanza kunywa Pombe mpaka ilipofika muda wa saa sita usiku wakaanza kupigana” aliongea Kamanda Zelothe Stephen
Akifafanua zaidi Bw. Zelothe alisema Mtuhumiwa alikiri kufanya tukio hilo, lakini haelewi walikuwa wanapigana kwa sababu gani, kwani alidai marehemu ndiye aliyekuwa na kisu na kuanza kumjeruhi mtuhumiwa jichoni ambapo naye akamnyang’anya hicho kisu na kuanza kumshambulia marehemu.
Kamanda Zelothe Stephen alitaja sehemu alizoshambuliwa kwa kisu marehemu kuwa ni tumboni, chini ya mbavu mkono wa kulia, kifuani kushoto, sehemu ya katikati katika paji la uso, pamoja na kupasuliwa na kisu katika mapaja yake yote mawili.
Aidha Bw. Zelothe Stephen alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa kwa mlinzi wa amani kwa kukiri kosa lake kama taratibu zinavyoelekeza halafu atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi katika Manispaa ya Dodoma mjini, katika misako ya iliyoendesha jana linawashikilia watuhumiwa Arobaini na Tatu (43) wa makosa mbalimbali ya uhalifu pamoja na Pombe ya Moshi Lita Mbili na mirungi bunda moja vilikamatwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments: