Na Mohammed Mhina, Handeni

Mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga Bw. Muhingo Rweyemamu, amepiga kambi kwenye mwambao wa misitu ya Kang'ata wilayani humo kukagua na kuona athari za uvamizi na ukataji miti ya uoto wa asili unaofanywa na wananchi kwa kisingizio cha kusafisha mashamba kwa ajili ya kilimo. 
Akiwa katika msitu huo, Mkuu huyo wa wilaya ya Handeni ameshuhudia uharibifu mkubwa uliotokana na uvamizi na ukataji wa miti ya asili katika misitu tengefu ya Kang'ata msitu ambayo ilikuwa ikihifadhi idadi kubwa ya makundi ya nyuki na kuvuta kiasi kikubwa cha mvua.

Kutokana na uharibifu huo mkubwa wa ukataji wa miti katika misitu hiyo, Bw. Muhingo amepiga marufuku utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti ya mkaa na mbao hadi hapo kamati maalumu itakapoweka utaratimu mpya wa utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti wilayani humo.

Akizungumzia uvamizi na uhalibifu huo wa uoto wa asili, Bw. Muhingo amesema kuanzia sasa mtu yeyote atakayeomba kibali cha kuvuna miti kwa ajili ya kupasua mbao ama mkaa ni lazima akaonyeshe shamba lake la miti kabla ya kufikiriwa kupata kibali.

Amesema hata baada ya kupata kibali hicho, mwombaji ambaye ni mwenyeshamba ni lazima ukaguzi ufanywe katika shamba la mhusika ili kujiridhisha kama kibali alichopewa amekitumia kwa kuvuna miti iliyopo katika shamba husika na ndipo apatiwe kibali kingine kwa ajili ya kusafirisha mazao hayo kutoka msituni hadi katika eneo la soko.

Bw. Muhingo amesema wilaya ya Handeni ambayo ina maeneo mengi ya misitu ya uwoto wa asili, hivi sasa iko hatarini kugeuka jangwa kama juhudi za makusudi za kukabiliana sasa na wavamizi wa misitu hiyo na kuikata hazitachukuliwa mapemba.

Amewataka viongozi wa Serikali za Vijiji na wananchi wenye maeneo makubwa ya ardhi, kuacha kuyauza maeneo hayo kwa wageni wanaodai wanataka maeneo kwa ajili ya kilimo kwani hata baada ya kupatiwa maeneo hayo wageni hao hukata mikaa na mbao akijifanya wanasafisha maeneo kwa ajili ya kilimo.

Akiwa katika harakazi za kuinusuru misitu wilayani handeni, Mkuu huyo wa wilaya, hivi karibuni alimkamata mmoja wa watumishi wa Idara ya Misitu akisafirisha kiasi kikubwa cha magogo yaliyovunwa bila ya kibali jambo lililopelekea kusimamishwa kazi kwa afisa huyo wilayani handeni.

Aidha Bw. Muhingo amewataka watumishi wote wa Idara ya Maliasili na Misitu wilayani humo kuwa waaminifu na waadilifu na kwamba kazi waliyonayo ni dhamana ya Watanzania wote na kwamba wao hawana mamlaka wa kutumia rasilimali hizo kwa kujinufaisha wenyewe na  familia zao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: