Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar
JESHI la Polisi Zanzibar limepiga marufuku maandamano na mihadhara ya aina yoyote visiwani hapa hadi hapo itakapotangazwa tena.
Taarifa ya Afisa Habari Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, imesema kuwa hatua hiyo inatokana na agizo la Serikali la kusitisha shughuli zote za mikusanyiko ya vikundi vya kidini vikiwemo vile vyenye usajili na ambavyo havina ili kuepusha uvunjifu wa amani.
Akisisitiza msimamo huo wa Jeshi la Polisi, Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa, amesema Jeshi la Polisi litachukua hatua kali kwa mtu ama kikundi chochote kitakachokaidi agizo hilo kwa lengo la kudumisha amani na usalamawa viisiwa hivyo.
Kamishna Mussa amesema Jeshi la Polisi limelazimika kutoa msisitizo huo kufuatia taarifa za viongozi wa kikundi cha Uamsho kuwatangazia wananchi kuwa kesho wangefanya mhadhara kwenye viwanja vya Lumumba kinyume na maagizo ya Serikali.
Amewataka Wananchi wakiwemo waumini wa dini zote kutojitokeza kushiriki mhadhara huo na mihadhara mingine itakayotangazwa katika kipindi hiki cha marufuku ya mikusanyiko ya aina hiyo.
Jana akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Zanzibar, Kiongozi wa Kikundi cha Uamsho Sheikhe Farid Hadi, alisema wangefanya mhadhara mkubwa hiyo kesho jioni na kufanya maandamano Jumanne ya Juni 26, mwaka huu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: