Na Mwandishi wa Jeshi la Polisi Zanzibar.
Michuano ya mpira wa ukutani (Squash) ya kutafuta mshindi wa miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar iIiyokua ianze jana Ijumaa Januari 13, 2012 kwenye ukumbi wa Polisi Ziwani mjini Zanzibar imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema michuano hiyo imeahirishwa kwa muda usiojulikana kutokana na ukata unaokikabili Chama cha Squash Zanzibar (ZSRA) (Zanzibar Squash Racket Association).
Akizungumzia hatua ya kuahirishwa kwa michuano hiyo, Katibu Mkuu wa ZSRA Haji Uzia Vuai, amesema kuwa michuano hiyo ambayo ilipangwa kufanyika kwa siku tatu imeahirishwa kutokana na Baraza la Michezo la Zanzibar kushindwa kutoa fedha za kuendeshea michuano hiyo kama ilivyopangwa hapo kabla.
Vuai amesema baadhi ya washiriki kutoka Tanzania Bara walishaanza kuwasili Zanzibar tayari kwa mashindano hiyo ambayo itapangwa tena baada ya kupatikana kwa ruzuku hiyo isiyozidi shingili milioni 2.
Hata hivyo Vuai ametoa wito kwa Serikali na wadau wa michezo wenye uwezo kukisaiidia chama chake ili kiweze kufanikisha michuano hiyo ambayo ipo kwenye ratiba ya sherehe za miaka 48 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Awali Vuai alimesema michuano hiyo ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka wakati wa sherehe za Mapinduzi, ilipangwa kumalizika kesho Jumapili Januari 15, 2012 kwenye ukumbi wa Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.
Amesema mshindi wa kwanza wa michuano hiyo atapata shilingi 200,000, wa pili atapewa shilingi 150,000 na shilingi 100,000 kwa mshindi wa tatu zawadi ambazo ziliahidiwa kutolewa na baraza la michezo la Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments: