Mbunge wa viti maalumu kupitia Chama Cha CHADEMA Bi. Regia Mtema amefariki dunia kutokana na ajali iliyotokea Ruvu, Pwani. Kwa mujibu wa taarifa iliyofikia Kajunason blog kutoka eneo la tukio zinasema kuwa Bi. Mtema alikuwa na familia yake akiwemo mama yake mzazi. Majeruhi wote wamepelekwa kwenye Hospitali ya Tumbi, kibaha-Pwani. Kwa habari zaidi na picha zitawaijia muda si mrefu.
---
Taarifa ya 
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinasikitika kutangaza kifo cha mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema (pichani) ambaye pia ni
Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani.


Katika uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.


Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum.


Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.


CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema, wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa chama na kwa taifa.


Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Imetolewa na: 
John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
Chadema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: