Hawa Ghasia
Watumishi wa Idara ya Afya jijini  Mbeya,  wameiomba Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kuingilia kati malalamiko yao dhidi ya ofisi ya utumishi ya jiji hilo kwa kile wanachodai kuwa ni kulipwa mshahara mdogo usiolingana na madaraja yao ya kazi.

Wakizungumza na Tanzania Daima, baadhi ya watumishi hao walisema kuwa wamekuwa wakizungushwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kwa muda mrefu wakifuatia malalamiko yao pasipo mafanikio.

Walisema baada ya kuzungushwa na ofisi ya mkurugenzi, waliamua kuhamishia malalamiko yao katika ofisi ya chama cha kutetea haki za watumishi wa idara ya afya halmashari ya jiji hilo, ili kufuatilia haki zao.

“Waraka wa serikali wenye kumb namba CAC./205/228/01/41 wa Julai 11 mwaka huu, unajieleza jinsi serikali ilivyofanya marekebisho ya mishahara ya watumishi wake. Kufuatia marekebisho hayo, kima cha chini cha mishahara kimeongezwa kwa asilimia 11 kutoka sh 135,000 hadi sh 150,000 kwa mwezi,” alisema mmoja wao akiungwa mkono na wenzake.

Watumishi hao ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, waliongeza kuwa kutokana na waraka huo, hawakustahili kulipwa mishahara yao kwa kiwango cha awali ambacho ni TGS A. 1  kwa kima cha chini badala yake wanatakiwa kulipwa kwa kiwango cha TGHS A.1 kwa mwezi, kama kima cha chini cha mshahara.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Kutetea haki za Watumishi, Odeni, (TALWGU) aliliambia gazeti hili kuwa malalamiko ya  watumishi hao wapatao 11 tayari alikwishayapokea.

Aidha, Odeni alisema ofisi yake itahakikisha inafuatilia kwa karibu madai ya watumishi hao ili waweze kupata stahiki zao lakini pia kurekebishiwa mishahara yao kulingana na madaraja walionayo.

Ofisa Utumishi wa Jiji la Mbeya, Komingo, hakupatikana ili kuzungumzia tuhuma hizo na hata simu yake ya kiganjani iliita bila majibu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: