TANZANIA
imekataa masharti ya Uingereza inayotaka nchi zinazotaka misaada yake
ziruhusu vitendo vya ushoga. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe alitoa msimamo huo leo Jijini Dar es Salaam
akisema huko ni kwenda kinyume na sheria na utamaduni wa nchi yetu
inayotambua ndoa ya mme na mke kama kiini cha familia. Membe alisema
hayo alipokuwa akizungumzia mkutano wa Jumuia ya Madola uliofanyika wiki
iliyopita Perth, Australia. Alitoa msimamo huo kufuatia kauli ya Waziri
Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuwa wana mpango wa kusitisha misaada
kwa nchi ambazo katiba na sheria zake hazitambui mashoga na ndoa zao.
"Nchi
yetu inaheshimu sheria na utamaduni wake hivyo hatupo tayari nchi
nyingine kutuwekea masharti kama hayo ya kuwa na uhusiano wa jinsi moja,
hili ni tamko hatarishi linaloweza kuvunja uhusiano na nje", Waziri
Membe aliwaambia waandishi wa habari. Alisema tamko hilo ni msimamo wa
chama cha Conservative na kibaya zaidi linatoka Uingereza ambako ndio
wenye Jumuia ya Madola hivyo linaweza kusababisha kuvunjika kwake na
Cameroun na nchi hiyo ndio watawajibika jumuia hiyo ikivunjika.
Alisema
miongoni mwa nchi 54 za Jumuia ya Madola kati yake nchi 13 ushoga ni
sehemu ya katiba yao wakati 41 hazina utamaduni huo hivyo msimamo wa
Tanzania ni kuwa na ndoa za jinsi mbili tofauti, kinyume na hapo
unafungwa kifungo miaka 30. Alisema kuendelea kukumbatia ushoga si jambo
zuri na si la kulishabikia hata kidogo vinginevyo wanaweza kujuta nchi
ikijihusisha na ushoga na kuukubali kupata misaada ya maendeleo.
"Tanzania
hatuwezi kuyumbishwa kwa masharti ya kipuuzi bora tuitunze nchi yetu.
Tanzania ni nchi maskini lakini kamwe haturuhusu kuingiliwa na nchi
nyingine. Kama ndio hivyo basi wakae na hela zao," alisema Waziri Membe
wizarani kwake.
Alisema
katika mkutano wa Madola, walijadili mabadiliko ya hali ya hewa ambapo
walibainisha nchi zinazotegemea mvua zichukue hatua gani kuishi bila
kuathiri hali hali ya hewa. Pia alisema walijadili kuhusu hatua za
kuchukua ili kuvisaidia visiwa vidogo kama Maldives vinavyoliwa na maji
ya bahari yanayojaa kufuatia mabadiliko ya hali ya hewa. Alisema
watakuwa na mkutano London Aprili mwakani kujadili mikakati hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: