Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi-Zanzibar
Jeshi la Polisi mkoa wa mjini Magharibi Zanzibar wamefanikiwa kukamata Bastola moja aina ya Star ikiwa na risasi sita.
Kamanda wa Polisi mkoa wa mjini Magharibi Unguja, Kamishna Msaidizi Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa silaha hiyo imekamatwa majira ya saa 8.00 usiku huko kwenye eneo la Sateni mjini Zanzibar baada ya Polisi kuwakurupusha watu watatu na kukimbia huku wakitupa kifurushi kilichokua na silaha hiyo.
Kamanda Aziz amesema awali Polisi walidokezwa kuwepo na wizi uliokuwa ufanyike kwenye ghala moja la kuhifadhia vinywaji baridi bapo waliweka mtego wa kuwanasa ambapo hata hivyo majambazi hayo yalitimua mbio baada ya kugundua kuwepo kwa askari.
Amesema Polisi hao walifukuzana na majambazi hayo huku wakifyatua risasi tatu hewani za kuwaonya kusimama lakini hawakufanya hivyo na wakatokomea gizani.
Kamanda Aziz amesema kuwa, kukamatwa kwa silaha hiyo kunatokana na taarifa sahihi na zilizotolewa kwa wakati sahihi juu ya kuwepo kwa mipango ya wizi katika ghala hilo na hivyo kuweka mtego.
Amesema taarifa sahihi zikitolewa kwa haraka na wakati sahihi huleta mafanikio. Hivyo amewaomba wananchi kuendelea kulisaidia Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa haraka na kwa wakati sahihi ili waweze kufanikisha kazi ya kupambana na wahalifu.
Hiyo ni silaha ya pili kukamatwa na Polisi mkoani humo katika kipindi kisichozidi wiki tatu ambapo silaha moja aina ya SMG ilikamatwa hivi karibuni baada ya majambazi watano kukimbia na kuitupa chini walipopambana na Polisi. Wakati huo huo, Mama mmoja mkazi wa Mombasa Zanzibar, Zimira Hashim Salum(26) anashikiliwa na Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa tuhuma za kumuua mpezi wake Faridi Iddi Othumani(32), kwa kumchoma kisu sehemu ya kifuani.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Kamishna Msaidi (ACP) Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 3.00 usiku huko kwenye eneo la Mombasa wakiwa katika nyumbani ya mkazi mmoja wa eneo hilo Bw. Athuman Omari Juma.
Kamanda Aziz amesema mtuhumiwa na marehemu walikuwa ni wapenzi na wamekuwa wakiishi kama mtu na mumewe kwa zaidi ya miezi mitatu sasa na chanzo chake hakijafahamika na Polisi wanaendelea na uchunguzi.
Katika tukio lingine, Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, wanachunguza chanzo cha kujinyonga kwa mkazi mmoja wa eneo la Mikunguni mjini Zanzibar Bw. Hassan Suleiman(22), aliyekutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga kwa kamba ya katani chumbani kwake.
Matukio ya kujinyonga katika Kisiwa cha Unguja hivi sasa yameonekana kushika kasi ambapo katika kipindi cha hivi karibuni watu wawili walijiua baada ya kujinyonga wenyewe.


Toa Maoni Yako:
0 comments: