JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Idara ya Habari - MAELEZO, S.L.P. 9142 - DSM, Simu 2122771/3,
Fax: 2113814, Mob 0784 44 82 21
E-mail: maelezopress@yahoo.com

DATE: 10/09/2008

Na Grace Gwamagobe-Maelezo

Makampuni na asasi zisizo za kiserikali nchini zimeombwa kuweka kipaumbele na kuona umuhimu wa kutoa misaada katika sekta ya elimu kama wanavyofanya katika sekta nyingine ili kuiinua na kuiboresha sekta hiyo.

Rai hiyo imetolewa jana na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkoani iliyoko wilaya ya Ilala Dar es Salaam, Mwalimu Pia Kuonga alipokuwa akipokea msaada wa madawati 80 kutoka kwenye kampuni ya simu za mkononi Vodacom Tanzania shuleni hapo.

“Makampuni yaone umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu na waweke kipaumbele huku kama wanavyochangia kwenye sekta nyingine mfano tunaona mpira ukichangiwa na makampuni mengi na pia mashindano ya umiss huwa yanapata udhamini mkubwa basi na huku kwenye elimu waone umuhimu wa kuchangia” alisema mwalimu Kuonga.

Mwailimu mkuu huyo aliongeza kuwa Vodacom imewasaidia kwani shule yake ilikuwa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati.Shule hiyo yenye wanafunzi 907 ilitakiwa kuwa na madawati 320 lakini ilikuwa na upungufu wa madawati 270.

“Shule ilikuwa na upungufu mkubwa wa madawati na tuliamua kuomba kwenye makampuni mbalimbali, tuliwaomba Vodacom madawati 70 walipotutembelea na kuona upungufu uliopo waliamua kutuongezea na kutupa madawati 80” aliongeza Mwalimu Kuonga.

Walimu na wanafunzi wa shule ya Msingi Mkoani wameipongeza Vodacom kupitia kitengo cha huduma kwa jamii (Vodacom Foundation) kwa kutoa msaada huo kwani madawati hayo ambayo yamepangwa darasa la nne, la tano na la sita yatawasaidia wanafunzi hao kwani walikuwa wanakaa chini na kuwapunguzia umakini wa kumsikiliza mwalimu.

“Tunaishukuru Vodacom tunaomba na makampuni mengine yajitokeze kutusaidia kwani watoto wanapata shida kukaa chini na kuandika ” alisema Mwalimu Khalid Semvua.

Wanafunzi nao waliupokea msaada huo kwa furaha, “Zamani tulikuwa tunakaa chini au dawati moja watu watano mpaka sita nitakuwa nawahi shule kuyatunza” alisema mwanafunzi wa darasa la tano, Gelda Modestus.

Aidha Meneja uhusiano wa Vodacom foundation, Bwana Yessaya Mwakifulefule,amesema wametoa msaada huo wa mdawati 80 yenye thamani ya shilingi milioni 6 kwa shule hiyo na wameahidi kuendelea kutoa msaada kwa shule hiyo.

Bwana Mwakifulefule alitoa wito kwa makampuni mengine binafsi yaanzishe kitengo cha kusaidia jamii kama ilivyo kwa Vodacom foundation ili kuzisaidia shule hasa hizi za kata ambazo ndizo zinakabiliwa na mapungufu mengi.

“Makampuni mengine nayo yangejitokeza tukasadiana katika kuiinua sekta hii ya elimu kwa pamoja, angalau kila kampuni ingejitolea kusaidia shule tano matatizo ya madawati na mengine yangekuwa yamekwisha kabisa” aliongeza Bwana Mwakifulefule.

Pia Meneja huyo alisema kuwa Vodacom imetenga kiasi cha shilingi milioni 43 kwa mwaka 2008/2009 kwa ajili ya ukarabati wa shule za msingi na za sekondari za Mafia na ujenzi wa maabara ambapo ujenzi huo pia upo chini ya mpango uleule wa Vodacom foundation.

Vilevile Meneja huyo aliongeza kuwa Vodacom chini ya mpango wa kusaidia jamii imeweza kuzisadia shule za msingi nyingi nchini kama vile Shule ya msingi Vijibweni, Shule ya msingi Mivinjeni, na Shule ya Msingi Temeke Wailes.
MWISHO.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: