"Makanisa yanashindwa kuwatumia waimbaji na kuwaona kuwa ni watu wa kawaida kumbe nao ni wahubiri wanahitaji sehemu mbali mbali sasa watu wengine wa mbali wakimwitaji mwimbaji ataondoka tu kwenda huko,"
"Waimbaji tutoe dhana ya kufikiria kwa tukirekodi albamu ndiyo tumetoka katika umaskini; na hii ndiyo inawafanya waonekane wanafanya biashara; tumtangulize Mungu aliyetuita kufanya kazi yake na yote tutazidishiwa,"
Hayo ni maneno aliyoanza kuongea Miriam Mhembelo mwimbaji wa nyimbo za injili hasa nyimbo za kusifu na kuabudu; wakati akifanya mahojiano na Jiachie jijini Dar es salaam wiki iliyopita.
Akielezea kwa ufupi historia ya maisha yake anasema, "Mimi ni mtoto wa tatu yaani mwisho katika familia yetu ambayo tupo wasichana wawili na kaka yetu mmoja ambaye pia ni wa kwanza.
Miriam mpaka sasa amefanikisha kurekodi albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la 'Niumbie Moyo safi' aliyoitengenezea Backyad Record's iliyoko jijini Dar es Salaam.
Akielezea alivyoanza kuimba Miriam anasema, "Nilianza kuimba tokea shule ya msingi Mgololo mkoani Iringa wakati huo nilikuwa naimba kwenye kwaya ya shule ambapo niliweza kufanya vyema.
"Pamoja na kuimba lakini nilipokuwa shule ya sekondari Lutengano, Mbeya nilitokea kuwapenda sana waimbaji wa nyimbo za injili 'Yoranda Adams, Nicol Milan, Cece Winers pamoja na Upendo Kilahiro na kunifanya nitamani siku moja niwe kama wao,".
"Kwaya ya Praise and Worship ya Kanisa la Dar es Salaam Pentecostal Church (DPC) lililoko jijini Dar es Salaam ndiyo chimbuko langu kubwa kwani baada ya kuokoka mwaka 2005 nilijiunga na kwaya hiyo na hapo ndipo nilipopata uzoefu mkubwa mpaka nilipoamua kuimba peke yangu.
Akizungumzia changamoto iliyonifanya mwimbaji kurekodi albamu yake peke yake Miriam anasema "Mungu amenipa kipaji cha kutunga nyimbo nyingi ndiyo maana nimeamua kupanua wigo na kuamua kutoa albamu yangu ambayo nimeipa jina la 'Niumbie Moyo safi' inayotarajiwa kuingia mitaani hivi karibuni.
"Napenda kumshukuru Mungu kwa jamii ilivyonipokea vizuri maana nimetoka kitofauti sana na kitu kinachonifanya niwe tofauti ni ubunifu wa ala za muziki zilizotengenezwa kwa ustadi mkubwa," anasema Miriamu.
Akizitaja nyimbo hizo ni pamoja na 'Nafsi yangu', 'Nijapo pita', 'Hakuna Mungu kama wewe Bwana', 'Nakushukuru Bwana', 'Onjeni Muone', 'Jehova Jire' mwingine ni 'Dare to believe' alioumba kwa lugha ya kiingereza pamoja na 'Niumbie Moyo Safi' uliobeba jina la albamu.
Akielezea mafanikio aliyoyapata mpaka sasa Miriam anasema, "Nyimbo zangu zimepata kibali hasa nyimbo zangu za 'Hakuna Mungu kama wewe Bwana', na 'Niumbie Moyo Safi' ambazo zimewasaidia kuwafungua watu wengi wenye matatizo kutokana na mashairi yaliyomo humo'.
Akizungumzia matatizo yanayorudisha nyuma muziki wa injili hapa nchini, anasema ni watu kukopi nyimbo na kuacha kununua nakala halisi (original) za waimbaji. Pia anasikitishwa na kilio cha waimbaji wenzake cha kutodhaminiwa na baadhi ya watumishi wa Mungu na kuonekana wao ni wapenda pesa.
"Ndugu mwandishi sipendi kusikia kilio cha waimbaji wenzangu wakisema kuwa hawadhaminiwi nalisema hili kwa uchungu kwa vile kila mmoja ameitwa katika nafasi yake, tupo tofauti sana kuna wengine wanategemea muziki, hivyo wanahitaji kuwezeshwa pale wanapotoa huduma.
"Ufike wakati watumishi wa Mungu watambue kuwa kuimba ni huduma kamili na inahitaji msaada; kuna wakati utatakiwa kwenda sehemu kuhudumu hivyo unatakiwa kuwezeshwa tujaliwe kimwili na kiroho, ili kesho twende sehemu nyingine kutangaza neno na watu wabadirike kupitia nyimbo zetu,"
Akitoa ujumbe kwa waimbaji wenzake, amewaomba waimbaji wote wa Tanzania wamwabudu Mungu katika roho na kweli na watafute maisha matakatifu maana bila kwa watakatifu hatuwezi kumwona Mungu.
Mwisho, hakupenda kuacha kutoa shukrani zake za kipekee kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na watu wote ambao ameweza kushirikiana nao katika shughuli zake za kutangaza injili kwa njia ya nyimbo.


NAMKUBALI SANA HUYO DADA. JULIUS WA JOHANESBURG.
ReplyDeleteDada Miriam ningependa kuwasiliana na wewe nitakupataje?
ReplyDeleteDEO.