Jumla ya wanawake wajawazito 154,699 mkoani Tabora sawa na asilimia 95 ya wanaohudhuria kliniki wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kupima virusi vya ukimwi mbapo kati yao 7058 wamegundulika kuwa na virusi vya ukimwi na 6343 wamepatiwa dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kati ya mwaka 2005 na mwaka huu.

Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi wa Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation( EGPAF) Tanzania Dr.Anja Giphart katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mratibu wa EGPAF Tabora Dr.Juma Songoro wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wadau wa afya ya Mama na mtoto uliofanyika mkoani Tabora leo na kufunguliwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

“Huduma za kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto( Prevention from Mother to Child Transmission,PMTCT) zilianza nchini Tanzania mwaka 2000,pamoja na jitihada zite ni asilimia 35 tu ya wamama wajawazito wamepatiwa ushauri nasaha na kupima afya zao,hii ina maana asilimia 65 bado
wanahitaji msaada kuweza kupata huduma hizi,” alisema Bi Giphart.

Bi.Giphart aliendelea kusema kuwa tangu shirika lake lianza kutoa misaada katika hospitali za mkoa wa Tabora, wilaya zote zimepiga hatua kubwa katika kutoa huduma kwa wagonjwa waathirika wa ukimwi na katika kuzuia maambukizo ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto(PMTCT).

Mkurugenzi huyo alisema kuwa EGPAF ilianza kuufadhili mkoa wa Tabora tangu mwaka 2004 kwa kutoa mafunzo maalum kwa wakufunzi na kwamba ufadhili ulikua katika nyanja ya kusaidia huduma za kuzuia maaambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuwasaidia wagonjwa na waathirika wa ukimwi.

Bi Giphart alimpongeza Mama Kikwete kwa kuanzisha ushirikiano kati ya EGPAF na Taasisi ya Wanawake na MaendeleoWAMA na kusema kuwa ushirikiano huo umeanza kutekelezwa kwa vitendo mkoani Tabora na kuongeza kuwa hadi sasa Tabora ina vituo vya afya zaidi ya 143 vinavyofadhiliwa na EGPAF vinavyotoa huduma ya kuzuia maambukizi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Mapema akifungua mkutano huo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alisema WAMA inatekeleza miradi ambayo inalenga kuboresha afya za vijana kwa kutoa elimu bora ya afya ya uzazi ikiwemo ile ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi na kwamba wadau mbalimbali likiwemo shirika la EGPAF wanashirikiana kutekeleza moradi ya kuboresha afya ya mama na watoto Tanzania .

Mama Kikwete alisema kuwa kati ya mwaka 1990 na mwaka 2004,vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vilipungua hapa nchini kutoka watoto 140 kato 1000 wanaozaliwa na kufikia 112 kati ya kila 1000 wanaozaliwa.

“Watafiti wanaonyesha kuwa matokeo haya yametokana na kutumika kwa vyandarua vyenye dawa,matone ya ya vitamini A,chanjo kwa watoto na unyonyeshaji bora wa maziwa ya mama,”alisema mama Kikwete.

Mama Kikwete alisema hali bado si ya kuridhisha nchini ambapo inakadiriwa kuwa wanawake 8,100 hufariki kila mwaka wakati wa ujauzito na vilevile watoto 45,000 hufariki kabla ya kutimiza mwaka mmoja na kwamba watoto 157,000 hufariki kabla ya kutimiza miaka mitano.

“Leo hii tunayo sababu ya kusema baadhi ya vifo hivi vinaweza kuepukika na hatuna budi kuviepuka,” alisisitiza Mama Salma na kusisitiza kuwa mama napokuwa mjamzito ni vyema utunzaji wa mtoto ukaanza mara moja na kwamba baba awe wa kwanza kushirikiana na mama kulea ujauzito kwa kuenda kwa wataalamu kupima afya zao na kurejea kwamashauriano katika kituo cha afya.

Kuhusu mpango wa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto PMTCT ambao umenza kutekelezwa na EGPAF kwa kushirikiana na WAMA, Mama Kikwete amesema kuwa mpango huo ni fursa ya pekee kunusuru maisha ya maelfu ya watoto hapa nchini.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi kuwapeleka watoto vituo vya afya kwaajili ya chanjo,kuwakinga na malaria kwa kutumia vyandarua vyenye dawa na kuwajali kwa lishe bora.

Mama Kikwete ambaye alikuwa mkoani Tabora kuzindua kampeni dhidi ya gonjwa la ukimwi kwa kutumia ngoma za jadi katika wilaya ya Nzega na kufungua warsha ya Afya ya mama na mtoto mjini Tabora tayari amerejea jijini Dar es Salaam.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: