Kigogo mmoja ambaye katika awamu hii ya nne ya uongozi wa nchi yetu ameukwaa wadhifa wa ukuu wa mkoa na kupangiwa moja ya mikoa ya pwani, amedaiwa kumpachika mimba mwanahabari mmoja mkoani kwake na kusamabaratisha ndoa ya mwandishi huyo.

Habari zinaeleza kuwa kabla ya kigogo huyo kumtundika mimba mwandishi huyo aliyekuwa ameolewa na mfanyakazi mmoja wa benki moja na wakabahatika kuzaa naye mtoto mmoja (majina yao tunayahifahi), alinogewa na penzi la mwanadada huyo jambo ambalo lilimhuzunisha mumewe na kuamua kutengana naye.

Baada kusambaratika kwa ndoa ya mwandishi huyo, imedaiwa kuwa kigogo huyo hivi sasa anaendeleza mapenzi yasiyo na kificho na paparazi huyo.
Imeelezwa kuwa, mara kwa mara dada huyo amekuwa akijivinjari nyumbani kwa kigogo huyo na kutumia gari analolitaka la bosi huyo, isitoshe anapewa heshima zote kama mke na askari wanaolinda usalama nyumbani kwake.

Mpashaji habari wetu amedai kuwa kigogo huyo baada ya kukolezwa na penzi la mwandishi huyo, tayari amemnunulia gari aina ya RAV 4 na kumuwezesha fedha za kujenga nyumba ya familia huku akifanya kila jitihada kulinda habari hiyo isifike kwa wake zake wawili ambao wanaishi nje ya mkoa huo.

Wakati kigogo huyo akitumbua maraha na mwandishi huyo, habari zinasema, wakeze wanaishi kwa dhiki kwani hivi karibuni mmoja wa wanahabari aliyetumwa na mkuu huyo kwenda mkoani kwake kuandika habari za maendeleo alisafiri na mke mmoja wa kigogo huyo kutoka wilayani kwake hadi Dar es Salaam na kuwalazimu kupanda daladala kwenda alipofikia.

Mkuu wa Mkoa huyo ambaye anatajwa kuwa ni kiwembe, awali aliwahi kuripotiwa na vyombo vya habari kuzama kwenye penzi zito la mwanahabari mwingine wa jijini Dar es Salaam ambaye alitaka kufunganaye ndoa lakini muda mfupi baadaye penzi hilo lilisambaratika baada ya mwandishi huyo kupata cheo cha uwakilishi bungeni.

Habari zilizopatikana hivi punde zinasema kuwa Machi 16, 2008 majira ya saa 2 usiku, mkuu huyo wa mkoa alinaswa na mwandishi wa habari hizi kwenye moja ya hospitali maarufu iliyopo makao makuu ya jiji analofanyia kazi, alimfikisha mwanadada huyo anayeandikia magazeti ya kampuni moja kubwa ya habari nchini ili aweze kujifungua.

Hata hivyo, jitihada za madaktari ziligonga ukuta baada ya kumfanyia upasuaji ambapo mtoto aliyetarajiwa alifariki dunia jambo ambalo linadaiwa kumhuzunisha kigogo huyo.

Habari zaidi zilizopatikana zinasema wanahabari wa mkoa huo, wamekuwa na neema kubwa tangu kuwasili kwa mkuu huyo mkoani humo na sasa humwita shemeji yao.

Alipopigiwa simu wiki iliyopita na mwandishi wetu na kuulizwa kuhusu habari hiyo alikana na kusema kuwa si za kweli. “Habari hizo si za kweli kabisa lakini kama mnajiamini mnaweza kuziandika,” alisema kigogo huyo wa mkoa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: