Nani zaidi? Ni swali ambalo sasa Watanzania wanajiuliza kutokana na jitihada kubwa anayofanya Rais Jakaya Kikwete ya kuifanya Tanzania kutambulika kimataifa ikilingashwa na Marais wa nchi nyingine katika Bara la Afrika.


Rais Kikwete mara baada ya kuchaguliwa na Watanzania kuongoza nchi, viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) nao walimchagua kuwa mwenyekiti wa umoja huo, hivyo kuiletea heshima kubwa nchi yetu.
Aidha, ujio wa marais zaidi ya 40 wa Afrika na wake zao na wageni wengine kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakaofika nchini Juni 2, mwaka huu katika mkutano wa Taasisi ya Leon Sullivan ni uthibitisho mwingine kuwa uongozi wa Kikwete kimataifa unakubalika.


Kwa mujibu wa Mratibu wa ujio huo wa Marais hao wa Afrika na wageni wengine, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (maelezo) Kassim Mpenda, Tanzania itapokea wageni wanaokadiriwa kufikia 4,000 na lengo kuu likiwa ni kuhimiza wawekezaji kuwekeza nchini hasa katika nyanja ya utalii.
Mpenda alisema hivi karibuni kuwa maandalizi ya ugeni huo mzito kutokea nchini, yanakwenda vizuri na kwamba timu nyingine inayoandaa mapokezi ipo mjini Arusha kwa kuwa nako wageni hao watatembelea.


Alitaja faida kubwa ya ugeni huo kuwa ni katika kujenga nyanja ya utalii kimataifa kwani mara wageni hao watakapoingia nchini, nchi yetu itatangazwa duniani kote na kutoa hamasa kwa watalii kuweza kututembelea.
“Kuja kwa wageni hao yaani marais pamoja na maofisa wengine ni faida kubwa sana kwetu kitalii na kiuchumi kwa sababu watafikia katika hoteli zetu na kulipa pesa, na Rais anajiandaa kuupokea” alisema Mpenda.


Aliongeza kuwa, kamati yake inajiandaa kuanza kutangaza ujio huo ili wananchi waelewe na kuwa tayari kuwapokea wageni hao wazito wa nchi yetu.


Mdau wa utalii nchini, Dk. Ngali Maita alisema Rais Kikwete ameonekana wazi kwamba nyota yake inang’aa kimataifa kutokana na majukumu mbalimbali anayoyapata kimataifa.


Akizungumza kwa simu juzi, Dk. Ngali alisema: “Hakuna haja ya kuogopa kusema ukweli, Rais Kikwete kwa kipindi kifupi sana ameliweka taifa juu kimataifa, leo hii ukiwauliza viongozi mbalimbali duniani kuhusu Tanzania, watakuwa wanaijua, ni kazi nzuri ya JK,” alifafanua mtaalamu huyo wa uchumi alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu ugeni huo unaotarajiwa kuwasili nchini.


Hivi karibuni Rais Kikwete alifanikisha ujio wa Rais wa taifa lenye nguvu za kiuchumi duniani, George Walker Bush wa Marekani ambaye alitoa misaada mbalimbali hasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.


Ujumbe huo wa Rais Bush, uliweza kutembelea Jiji la Arusha na kuona vivutio mbalimbali vya kitalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro.


Aidha, Rais Kikwete pia ameonekana ni zaidi baada ya kufanikiwa kutatua mzozo wa kisiasa ulioibuka nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu kati ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Mteule, Raila Odinga.Katika mzozo huo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Kenya, Bw. Samweli Kivuitu alisema alilazimishwa kumtangaza Kibaki hali iliyosababisha ghasia na kuripotiwa kuwa watu wasio na hatia zaidi ya 1,000 walipoteza maisha na mali za mamilioni ya shilingi kuteketezwa moto.


Rais Kikwete pia aliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuungana na Majeshi ya Umoja wa Afrika kwenda Comoro kumng’oa Kanali Mohamed Bacar ambaye alijitangazia Urais wa kisiwa kidogo cha Anjoun, visiwani humo.


Hivi sasa JK anatakiwa kwa udi na uvumba nchini Zimbabwe ambako kuna mgogoro mkubwa wa kisiasa kati ya Rais Robert Mugabe na Tsvangirai anayedai kushinda uchaguzi mkuu wa Urais. Mshindi wa urais wa uchaguzi huo hadi jana alikuwa bado kutangazwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: