Mauaji ya kikatili ya kuchinjwa kama kuku mtoto pekee kwa wazazi wake, Salome Yohana (3) yameumiza wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam na hata nje ya jiji na vitongoji vyake na wameiomba serikali kuwachukulia hatua kali wote waliohusika na kitendo hicho.

Akimsimulia safu hii ya HABARI NA MATUKIO jinsi Salome alivyotoweka nyumbani na kukutwa amechinjwa, mama mzazi wa mtoto huyo, Upendo Dustan (27) alisema kuwa siku hiyo ya Ijumaa wiki iliyopita majira ya saa 2.00 usiku aliandaa chakula wakala na mwanaye ambaye baadaye alikwenda kucheza nje na mtoto wa jirani yao.
(Mtoto Ramadhani, siku alipokutwa na kichwa, akiimpa onyo mwandishi kuwa naye hana muda mrefu wa kuishi)
“Wakati mwanangu anaendelea kucheza nje niliamua kuweka neti kitandani ili aje alale na kabla sijamaliza kutandika akaja baba yake akaniuliza alipo mtoto nilimfahamisha kuwa anacheza nje ambapo alikwenda kumuangalia, baada ya muda alirudi ndani akaniambia hajamuona.
“Hata hivyo, shangazi yangu aitwae Furaha Majani ambaye tulikua naye ndani alitoka nje kumtafuta bila mafanikio hali hiyo ilinipa wasiwasi na kunifanya nitoke nje kumuangalia lakini nami sikumuona.
“Baadaye tuliamua kumtafuta kwa majirani lakini hatukumuona, ilibidi tutoe taarifa katika msikiti wa hapa karibu ambapo majira ya saa 3.45 usiku viongozi walitangaza lakini hatukumpata.
“Nilianza kupotelewa na nguvu, hata hivyo, nikiwa na wenzangu tuliendelea kumtafuta hadi saa nane usiku hatukumpata, ilitubidi tupumzike kesho yake asubuhi tulijipanga kumtafuta ambapo wengine walienda vituo mbalimbali vya polisi na baadhi wakaenda kumtafuta hospitalini ikiwemo ya Muhimbili lakini hawakumuona.
(Jirani na aliposimama jamaa ndipo mtoto alipochinjiwa)
Watu walianza kusambaa, lakini katika kundi letu akajitokeza mtoto mmoja akatuuliza kama tumeshampata Salome, nikamueleza bado, alitueleza kuwa kuna kiwiliwili cha mtoto kimeokotwa, alitueleza kilipo na nguo alizovaa, tuliamini ndiye yeye, nguvu ziliniishia nikajitahidi kufika eneo la tukio, nilikuta ni yeye nwanangu Salome (machozi).
“Ilibidi nipige simu polisi ambao walipofika eneo la tukio, walikisaka kichwa cha mwanangu hadi ndani ya choo bila mafanikio na baada ya muda mfupi tulipigiwa simu kuwa kuna kijana mmoja kakamatwa Muhimbili na kichwa cha mtoto, tulikwenda kukiona tulitambua kuwa ni cha mwanangu.

WAGENI WA SEGEREA “Hapa Segerea tulikuja wiki moja iliyopita kumsalimia shangazi ambapo tulimuacha marehemu, mimi na mume wangu tulirudi nyumbani kwetu na Ijumaa tulifika tena hapa na usiku kabla hatujaondoka kurudi kwetu ndipo Salome akawa ametekwa na watu tusiowajua,” alisema Bi. Upendo.
(Marehemu akiwa na wazazi wake enzi za uhai wake)
Baba wa marehemu, Bw. Mussa alipohojiwa alisema kwa kuwa watuhumiwa wamekamatwa hana la kusema isipokuwa kuiachia serikali ili sheria ichukue mkondo wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi na jana wananchi mbalimbali jijini Dar es Salaam kuhusu tukio hilo, walisema kuwa haingii akilini mwa binadamu kuona mtoto mdogo kama Salome ambaye hana hatia anatekwa na kuchinjwa.
Mkazi mmoja wa Tabata, Bw. Selemani Ali Mtula alisema kuwa mauaji ya mtoto huyo yanatia shaka na inawezekana kuna kundi kubwa la watu wanaofanya unyama huo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: