*** TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI***


Pichani ni Mbunge wa kigoma kaskazini (Chadema) Mheshimwa Zitto Kabwe.

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda hajasema kuwa Tanzania iko tayari kupeleka jeshi Zimbabwe kama ilivyoandikwa kwa makosa katika gazeti la kila siku la Kiingereza linalochapishwa Dar es Salaam THE CITIZEN toleo la leo (Ijumaa Apr. 11, 2008).
Alichosema Waziri Mkuu katika Bunge mjini Dodoma jana (Alhamisi Apr. 10, 2008) asubuhi wakati wa kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu kujibu swali la Mbunge Zitto Kabwe (Chadema) ni kwamba kama ni kupeleka jeshi Zimbabwe basi uamuzi huo utakuwa wa Umoja wa Afrika (AU).
"Kama ni lazima kupeleka jeshi mimi nasema kama ni lazima AU nina hakika itakaa chini itatazama what to do (nini cha kufanya) na kama hapana budi watafanya hivyo," alisema.
Katika swali lake kuhusu hali ya Zimbabwe, Mbunge Kabwe aliuliza kutaka kujua kuwa endapo Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) iliyotakiwa ikutane kujadili suala la Zimbabwe itaamua kupeleka jeshi la kulinda amani nchini humo kufuatia utata katika matokeo ya uchaguzi, Tanzania itakuwa tayari kupeleka jeshi kama ilivyopeleka Comoro.
Katika gazeti hilo la THE CITIZEN, kwenye habari ya ukurasa wa kwanza, iliandikwa kwa kichwa cha maneno "Dar ready for military action in Zimbabwe", ikimaanisha kuwa Tanzania iko tayari kuchukua hatua za kijeshi Zimbabwe, jambo ambalo kamwe halikuzungumzwa na Waziri na Waziri Mkuu Pinda.
Swali la Mbunge Kabwe na majibu ya Waziri Mkuu, kama yalivyonakiliwa kama yalivyo, katika taarifa rasmi ya Bunge ambayo hupatikana Ofisi ya Bunge ni kama ifuatavyo:-
"MHE. KABWE ZUBERI ZITTO: Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Zimbabwe. Mheshimiwa Waziri Mkuu (nchi) yetu imekuwa katika juhudi mbalimbali za kimataifa za kuleta amani, leo tunavyozungumza ni wiki ya pili toka uchaguzi ufanyike Zimbabwe matokeo hayajatangazwa na kuna juhudi dhahiri kabisa Chama cha ZANU-PF ambacho ni marfiki wa chama chako kukataa kukubaliana na matokeo yatakavyokuwa. Serikali ya Tanzania inasemaje kuhusiana na uchaguzi wa Zimbabwe?
WAZIRI MKUU: Haya ningekuwa na uwezo wa kukuuliza na mimi ningesema Kabwe unanishauri nini? Tuseme nini wote (Kicheko/Makofi).
Mheshimiwa Spika, suala la Zimbabwe ni kitendawili si kwa Serikali ya Tanzania lakini ninaweza kusema kwa Afrika yote na ninaweza kusema hata kwa International Community yote, si jambo linalopendeza hata kidogo yaani halipendezi hata kidogo. Na unapokwenda kumsaidia mtu si lazima aonyeshe dalili za kukuomba kwamba Mzee njoo unisaidie kama hujaombwa unaweza ukainuka tu akakwambia nani kakutuma?
Kwa hiyo, unalolisema ni concern (kuhusika) kwa kila mtu sisi wote hapa we are very much concerned (tunahusika sana) lakini aah! mimi nasema ngoja tungoje tuone litakalotokea ni nini.
Tunaye Mwenyekiti wa Nchi za SADC (Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika) kwa hiyo nadhani pengine inaweza ikawa ni kiungo cha karibu zaidi kuliko pengine hata Chairman (Mwenyekiti) wa AU (Umoja wa Afrika). Lakini ni kweli Tanzania sisi tume play role (shiriki) kubwa sana kwa uhuru wa Zimbabwe aah! sasa tungoje tuone litatokea nini maana mimi sina jibu la harakaharaka kwenye eneo hili hata kidogo. (Makofi)
MHE. KABWE ZUBERI ZITTO: Mheshimiwa Spika, mara nyingi tumekuwa tukingoja matokeo yake maafa yanatokea na hiyo huo ni mfano ambao ulitokea Kenya.
Lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu keshokutwa SADC wanakutanaa iwapo SADC wataamua kupeleka jeshi Zimbabwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaweka amani na aliyeshinda uchaguzi anapewa haki yake ya kushinda. Tanzania itakuwa tayari kupeleka Jeshi kama ilivyopeleka Comoro? (Kicheko).
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri umeliweka vizuri kwamba je kama itaonekana kwamba aliyeshinda uchaguzi na Serikali inaombwa kwenda kuhakikisha huyo aliyeshinda na mifumo mingine inaendelea kazi zake kwa salama bila ya matatizo je Serikali itakuwa tayari kuridhia jambo hili.
Kwa sababu msingi wake mkubwa unanzia hapo lakini so far (mpaka sasa) hatujui nani mshindi lakini tuna taarifa za juu juu tu juu ya jambo hili kwa hiyo mimi nadhani tungoje International Pressure (shinikizo la kimataifa) na mimi najua ipo kubwa, tutakapopata a breakthrough (ufumbuzi) na kwa kweli kama ni lazima kupeleka jeshi nasema kama ni lazima AU nina hakika itakaa chini itatazama what to do (nini cha kufanya) na kama hapana budi watafanya hivyo. (Makofi)"
Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021,
DAR ES SALAAM.
Ijumaa Apr. 11, 2008
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: