Chato, Geita: Tanzania leo imeadhimisha miaka mitano tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli, kwa maadhimisho ya kitaifa yaliyofanyika nyumbani kwake wilayani Chato mkoani Geita.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, amewasili na kuongoza maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi.

Maadhimisho hayo yamepambwa na Misa Takatifu iliyofanyika nyumbani kwa hayati Magufuli, huku Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kushiriki, hatua inayodhihirisha heshima kubwa ambayo taifa linaendelea kumpa kiongozi huyo aliyewahi kuongoza nchi kwa kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu”.

Katika kuelekea kilele cha kumbukizi hizo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Geita, Jesca Magufuli, jana aliongoza matembezi maalum ya hisani jijini Chato kwa lengo la kumuenzi baba yake. Matembezi hayo yalihusisha wananchi wengi walioshiriki kwa ari kubwa kuonesha upendo na mshikamano.

Mbali na matembezi hayo, Jesca alitembelea Gereza la Wanawake Chato na kutoa msaada wa mahitaji muhimu kwa wafungwa. 

Aidha, alifika katika Hospitali ya Wilaya ya Chato na kuwafariji wagonjwa kwa kuwapatia vifaa na misaada mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuwajali wanyonge katika jamii.

Maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa la kukumbuka mchango wa hayati Magufuli katika maendeleo ya taifa, huku wananchi wakitumia fursa hiyo kutafakari misingi ya uzalendo, uwajibikaji na uchapakazi aliyoisimamia wakati wa uongozi wake.

Chato imeendelea kuwa kitovu cha kumbukizi hizo, ikikusanya Watanzania kutoka maeneo mbalimbali kuenzi maisha na urithi wa kiongozi huyo, huku kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu” ikiendelea kuishi mioyoni mwa wengi.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: