
Watu watatu akiwemo mwanaume mmoja na wanawake wawili, wakazi wa Kitongoji cha Goye, Kijiji cha Goye, Kata ya Ndato, Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, wamefariki dunia baada ya kupigwa na radi iliyotokea wakati wa mvua kubwa walipokuwa shambani.
Kwa mujibu wa ndugu wa familia, waliotambuliwa kufariki dunia ni Wilson Sanga (27), Sikuzani Tumaini Sanga (39) na Lucia Joseph Mlumbe (49).
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba mchana Februari 19, 2026, wakati watatu hao walipokuwa wakivuna mahindi shambani. Inadaiwa kuwa mvua kubwa ilipoanza kunyesha huku ikiambatana na radi, waliamua kujificha chini ya mti wa asili ili kujikinga, ndipo radi ilipowapiga na kusababisha vifo vyao papo hapo.
Mwenyekiti wa Kitongoji alithibitisha kuwa baada ya tukio hilo kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Kijiji, uongozi wa kijiji uliwasiliana na Jeshi la Polisi ambalo lilifika eneo la tukio na kuuchukua miili ya marehemu. Miili hiyo ilipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Makandana iliyopo Tukuyu kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitabibu.
Wakati huohuo, taratibu za mazishi zinaendelea huku familia na wananchi wakisubiri taarifa rasmi ya uthibitisho kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kuhusu chanzo kamili cha vifo hivyo.
Tukio hilo limeibua wito kwa wananchi kuchukua tahadhari zaidi wakati wa mvua zenye radi na kuepuka kujikinga chini ya miti, hatua inayotajwa kuongeza hatari ya kupigwa na radi.


Toa Maoni Yako:
0 comments: