Serikali imewataka viongozi wa kisiasa pamoja na watendaji wa serikali kutotumia madaraka yao vibaya kuwanyanyasa na kuwasumbua wawekezaji wazawa waliowekeza ndani ya nchi.
Aidha viongozi hao wametakiwa kuwaheshimu na kuwajengea mazingira rafiki yatakayowawezesha kufanya biashara zao kwa amani ili kuweza kukuza uchumi wa taifa na kuongeza ajira kwa vijana.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Prof. Adolf Mkenda mkoani Simiyu, wakati wa sherehe za uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji wa mkoa huo pamoja na tovuti ya Mkoa.
Prof. Mkenda amewasihi viongozi wote wa serikali ngazi za mikoa na wilaya nchini kujivunia uwepo wa wajasiriamali na wafanyabiashara wakubwa ambao ni wazawa kwani wao ni chachu ya kuongeza kwa ajira za vijana.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Prof. Godius Kahyarara (anayetazama kamera) akibadilishana mawazo na baadhi ya viongozi wa mkoa wa Simiyu nje ya ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi wakati wakimsubiri mgeni rasmi kuwasili kwenye sherehe za uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji na tovuti ya mkoa wa Simiyu.(Picha zote na Thebeauty.co.tz).
Amesema kuwa si vyema wafanyabishara kutukanwa, kutolewa lugha zisizokuwa sahihi na kuonekana kama wana uadui na serikali, na badala yake watukuzwe ili kuweza kulipa kodi pamoja na kufuata sheria na taratibu za nchi.
“Hawa wafanyabishara hasa wazawa na wajasiriamali tuwaone kama wenzetu, ndugu zetu na watu muhimu, kwani wameajiri vijana wetu, wanalipa kodi ili nchi ipate maendeleo, lakini wanatekeleza kauli mbiu ya Rais, Tanzania kuwa nchi ya viwanda, tuwathamni” alisema Prof.Mkenda.
Katibu Mkuu huyo amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji wakubwa na wadogo kwa ajili ya kujenga viwanda.
Awali akizungumza katika sherehe hizo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka amesema kuwa ili Tanzania iweze kufanikiwa katika azma yake ya kuwa na viwanda lazima serikali iwekeze kwanza katika utafiti wa fursa zilizopo.
Amesema kuwekeza katika utafiti utasaidia kutoa uthubutu wa kufanya na kutenda mambo mbalimbali yatakayoifanya nchi kuwa na uchumi wa kati na kuwaletea wananchi maendeleo.
“Nchi hii tusingelihitaji kuona wakuu wa mikoa kuwa wabobezi katika kila sekta na badala yake wawaache wataalam na watafiti wafanye kazi zao kitaalamu ili kuepuka mvurugano wa shughuli za kimaendeleo ndani ya nchi” amesema Mtaka
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne A. Sagini akitoa utambulisho wa meza kuu na maelezo ya lengo la mwongozo wa uwekezaji katika sherehe hizo zilizofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki Bariadi, Mkoani Simiyu.
Kwa upande wake Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Uchumi (ESRF) Dk. Gratian Bamwenda, amesema kukamilika kwa utafiti huo mkoani Simiyu utatoa fursa kwa wananchi na wafanyabishara kutambua wapi kuna fursa sahihi na haraka kuwekeza.
Utafiti huo ulifanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Uchumi (ESRF) kati ya mwezi Januari na Februari mwaka huu mkoani humo kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ambapo zaidi ya shilingi Milioni 60 zilitumika katika utafiti huo na kubaini uwepo wa fursa 26.
[caption id="attachment_919" align="aligncenter" width="1404"]
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) nchini ambao ndio wafadhili wa utafiti huo, Awa Dabo akitoa salamu za UNDP wakati wa sherehe za uzinduzi wa mwongozo wa uwekezaji mkoani Simiyu.
Toa Maoni Yako:
0 comments: