Mgomo wa madereva uliodumu kwa siku mbili, jana ulisitishwa baada ya kikao baina ya viongozi wao na viongozi wa Serikali kuhusu namna ya kushughulikia madai yao.

Kwa muda mrefu sasa, madereva wamekuwa kwenye mvutano na Serikali kuhusu uhakika wa ajira zao na pia tangazo la Serikali linaloweka sharti la kuwataka wapate mafunzo ya muda mfupi na kufanyiwa majaribio kila wakati leseni zao zinapoisha muda.

Tangazo hilo linahusu madereva wenye leseni za daraja E, C3, C2, C1 na C kuhudhuria mafunzo hayo ya lazima kabla ya kupewa leseni mpya.

Madereva hawana tatizo na mafunzo hayo, bali wanadai kuwa bila ya kuwa na ajira ya uhakika, kuhudhuria mafunzo hayo kutawafanya wapoteze ajira zao kwa kuwa waajiri hawatavumilia magari yao kutofanya kazi kwa kipindi hicho.

Madereva walifanya mgomo kama huo Aprili 9 na kusababisha usafiri kusimama kwa takriban saa tisa kabla ya kupewa suluhisho la kisiasa kuwa Serikali itahakikisha wanakuwa na mikataba ya ajira na pia kutangaza kufuta kuanza kutumika kwa sharti la kuwalazimisha kupata mafunzo na kuondoa tochi za kung’amua kasi ya magari.

Siku chache baadaye, Serikali ikatangaza kuwa suala la mafunzo kwa madereva liko palepale na haitarudi nyuma katika kutekeleza uamuzi wake, kitendo ambacho kiliwafanya madereva kujipanga upya na kutekeleza tena azma yao ya kugoma juzi na jana. Inavyoonekana ni kama Serikali haina majibu ya uhakika kuhusu suluhisho la madai ya madereva licha ya suala hilo kuwa la muda mrefu na ambalo ni mtambuka kutokana na ukweli kuwa linahusisha wizara nne tofauti.

Wakati yakitakiwa majibu ya haraka ili madereva wasitishe mgomo kwa muda na pia ukitakiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kupata suluhisho la muda mrefu, ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe waliofika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) jana kujaribu kutuliza madereva, wakati Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga alifika hapo wakati suluhisho hilo la muda limeshapatikana. Tulidhani kuwa mawaziri wote ambao wizara zao zinahusika kwa njia moja au nyingine kwenye sakata hilo, wangekwenda kwa pamoja UBT kueleza mpango wa Serikali au mazungumzo yanayoendelea, lakini si wao wala manaibu waliofanya hivyo ukiondoa Mahanga ambaye pia alichelewa.

Madai ya madereva ni ya msingi kwa maana kwamba wanadai ajira zao zirasimishwe, kitu ambacho kitaisaidia Serikali katika mambo mengi kama vile kudhibiti tatizo hilo la ajali, kukusanya mapato kwa njia ya kodi, kufuatilia taarifa za utendaji wao na pia kuwawezesha kushughulikia masuala yao kimaisha kama vile hifadhi ya jamii na kupata mikopo.

Katika madai kama hayo ya msingi, hatuoni ni kwa nini hadi leo Serikali inashindwa kupata njia itakayorasimisha ajira hizo, ili kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya kazi na pia Serikali inufaike na taarifa muhimu za madereva na ajira zao, kodi na masuala mengine ya kimaisha na kiuchumi.

Kila mwaka, bajeti ya Serikali hukosolewa kwa kushindwa kupanua wigo wa kukusanya kodi. Iweje leo wametokea madereva ambao wanaiambia Serikali kuwa kodi inaweza kukusanywa kutoka kwao kwa njia ya kuwa na mikataba ya ajira, halafu Serikali ikashindwa kuchukua hatua za haraka?

Tunazidi kuikumbusha Serikali kuwa inapaswa kushughulikia matatizo ya madereva na kupata suluhisho la kudumu na si la ahadi za kusitisha matumizi ya masharti mapya na kuondoa tochi kama ilivyokuwa mwezi uliopita.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: