Jana nikapata habari kuwa Mhe. Edward Lowassa amezungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini - amekana kuhusika kwake na Richmond. Nikashtushwa sana na hili. Nikajiuliza hivi ni nini kinataka kutokea kwenye siasa za nchi yangu? Mjadala wa Richmond ulifungwa Bungeni miaka 7 iliyopita, je inabidi ufunguliwe upya, na watu wapya tutafakari upya? Maana kuna minong'ono kuwa Mhe. Lowassa anataka kuwania Urais mwaka 2015, na ana mpango wa kutangaza nia muda si mrefu. 

Nikajiuliza, ni kwa nini imemchukua Mhe. Lowassa zaidi ya miaka saba kujibu hadharani kuwa hakuhusika na Richmond? Kwa nini anatamka maneno haya leo na kwa nini hakujitetea Bungeni siku ile alipojiuzulu? Nakumbuka siku ile alisema tatizo ni uWaziri Mkuu, kwa nini hakufafanua na alikuwa na fursa hiyo kama 'primus inter pares (first among equals)?' Kipindi fulani alisemekana kuwa ni 'gamba' na lingepaswa kuvuliwa...likaishia kiunoni! Ni kwa nini halikuvuka? Maswali haya sijawahi kuyapatia majibu.

Hivi ilikuwaje Rais wa Nchi, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, Kamati ya Wabunge Wote wa CCM Bungeni, na mamlaka zote za kiserikali kushindwa kumlinda Waziri Mkuu wake dhidi ya tuhuma za kuhusika kwake kwenye Richmond mwaka 2008? 

Maana kwenye siasa za mabunge yanayofuata mfumo wa Westminster, Waziri Mkuu ni 'primus inter pares', kwamba ana fursa ya kwanza ya kuzungumza kwenye mijadala Bungeni na ana-enjoy nguvu ya kuwa na majority bungeni kuendesha mambo ya serikali na kutawala mijadala na maamuzi. Ilikuwaje Chama kilimuacha Waziri Mkuu wake akaanguka? 

Ilikuwaje? Maswali: je kulikuwa na ukweli dhidi yake kuhusiana na tuhuma za Kamati? Ama Kamati ilitumika vibaya na mahasimu wake? Yeye amekana, sasa wanakamati inabidi wamjibu watuweke wazi, na wamjibu kwa uwazi bila kuficha, maana kama alionewa ijulikane na sisi tuliohuzunishwa ama kufurahishwa na Bunge wakati ule tuujue ukweli. 

Yeye anasema hakuhusika na ndiyo maana Kamati ya Mwakyembe haikuona haja ya kumwita kumhoji. Ukweli tunauhitaji sana leo kuliko jana. Ukweli huu ni haki yetu.
Kama Kamati ilimuonea, basi imuombe radhi na ituombe radhi watanzania wote. 

Kama kweli Mhe. Lowassa atagombea Urais Twentyfifteen, itakuwaje kwenye mijadala ya uchaguzi na CCM itasimamaje (kama itampitisha kuwa mgombea) kumuombea kura wakati ilimuangusha Bungeni kutoka kwenye nafasi nyeti ya Uwaziri Mkuu? CCM itatoa majibu gani kuhusu kwa nini ilimuita 'gamba' na ikatangaza hadharani kuanza mchakato wa kuvua magamba (ambao haukukamilika). 

Nilisema jana, Mhe. Lowassa amefungua pandora box, na kama atatangaza kweli kuwania Urais, inabidi haya mambo yawekwe wazi, yamalizwe, maana hauwezi jua ya kesho - ikitokea akawa mgombea wetu, tutaanzia wapi kumnadi na kusema ni mtu safi, muadilifu, anayechukia rushwa na ubadhirifu na kwamba anafaa kuwa Rais, wakati juzi tulisema hafai kuwa Waziri Mkuu na tukamtoa? 

Nilisema jana kuwa , CCM haipaswi ku-risk kuteua wagombea wenye mambo mengi ya kutolea maelezo kwa wananchi, ikifanya hivyo itaangushwa asubuhi ya saa nne. Watanzania wa leo siyo wa juzi.

Ni Mimi Maige Saganda
Bariadi - Simiyu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: